Saudi Arabia kufanya majaribio ya teknolojia 32 kuelekea ibada ya hija 1445

Saudi Arabia kufanya majaribio ya teknolojia 32 kuelekea ibada ya hija 1445

Saudi Arabia inalenga kupokea wageni Mahujaji wa Kiislamu zaidi ya milioni mbili wakati wa hija ya mwaka huu.
Baadhi ya waumini wa Kiislamu wakishiriki ibada ya hija nchini Saudi Arabia./Picha:Reuters

Kwa mara ya kwanza, Saudi Arabia itatumia mchanganyiko wa lami na mpira kwa ajili ya watembea kwa miguu ili kuwakinga na joto kali linalokabili eneo hilo.

Siku ya Alhamisi, Waziri wa Huduma za Uchukuzi wa Saudi Arabia, Saleh bin Nasser Al-Jasser, alitangaza kuwa jumla ya teknolojia mpya 32 zitafanyiwa majaribio wakati wa msimu wa hija ili kukidhi mahitaji ya kila siku wakati wa hija hiyo.

Al-Jasser aliweka wazi kuwa teknolojia hizo zitatumika kwa mara ya kwanza kwenye barabara, hususani mchanganyiko wa lami na mpira kwa ajili ya njia ya watembea kwa miguu wakiwemo mahujaji.

Vile vile amedokeza kuwa kutandazwa tabaka jeupe kutasaidia kupunguza joto kwa zaidi ya nyuzi joto 15, likiwemo eneo linalopakana na Msikiti wa Namira huko Arafat, pamoja na kuongezeka kwa matumizi ya ndege zisizo na rubani kukagua na kutathmini mtandao wa barabara.

Waziri huyo ameongeza kuwa mfumo wa usafiri wa nchi hiyo umejipanga kikamilifu kuhakikisha mahujaji wanasafirishwa salama kupitia njia mbalimbali za anga, nchi kavu, baharini na reli, toka wanapowasili Saudi Arabia kwa ajili ya ibada ya Hija na kuhakikisha pia wanaondoka salama.

‘Viwanja sita vya ndege katika Ufalme vimeanzishwa ili kupokea ndege za mahujaji, vikipanga safari za ndege 7,700 na kutoa viti milioni 3.4 ndani ya ndege,” alisema.

Pata Habari Zaidi kupitia WhatsApp channels

TRT Afrika