Wanafunzi watatu wa chuo kikuu wenye asili ya Kipalestina walijeruhiwa Jumamosi kwa kupigwa risasi katika mji wa kaskazini mashariki mwa Marekani wa Burlington, Vermont, katika kile polisi walisema kilionekana kuwa "uhalifu unaochochewa na chuki."
Mshambuliaji huyo ambaye bado hajakamatwa , alielezwa na polisi kuwa ni "mzungu mwenye bunduki."
"Bila kuzungumza," polisi walisema, "alifyatua angalau risasi nne kutoka kwa bastola na inaaminika alikimbia kwa miguu."
Tukio hilo lilitokea huku kukiwa na mvutano mkubwa, na vurugu za mara kwa mara, kwenye kampasi za vyuo vikuu na kwingineko nchini Marekani kutokana na vita vya Israel dhidi ya Wapalestina huko Gaza.
Taarifa ya polisi ilisema wawili kati ya waathiriwa walikuwa katika hali nzuri, na wa tatu alipata "majeraha mabaya zaidi." Ilisema wawili ni raia wa Marekani na mmoja mkazi halali.
Ingawa hakukuwa na thibitisho rasmi la nia ya mshambuliaji huyo, polisi walisema kwamba vijana wawili walikuwa wamevaa keffiyeh, skafu ya jadi nyeusi na nyeupe ya Wapalestina.
Na taarifa kutoka kwa mkuu wa polisi wa Burlington Jon Murad ilisema: "Katika wakati huu wa hamaki nyingi , hakuna mtu anayeweza kutazama tukio hili na kutoshuku kuwa lilikuwa uhalifu unaochochewa na chuki."
Aliongeza: "Sasa waathiriwa wako salama na wanapata huduma za matibabu, kipaumbele chetu kinachofuata ni kumtambua, kumtafuta na kumtia nguvuni mtuhumiwa."
'Inashangaza na inasikitisha sana'
Taarifa kutoka kwa msemaji wa familia za waathiriwa ilisema wote watatu walikuwa wamehitimu katika Shule ya Ramallah Friends, shule ya kibinafsi ya Quaker katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa, na sasa wanahudhuria vyuo vikuu tofauti kaskazini Mashariki mwa Marekani.
"Kama wazazi," ilisema taarifa hiyo, "tumesikitishwa na taarifa za kutisha kuwa watoto wetu walilengwa na kupigwa risasi. Tunatoa wito kwa vyombo vya sheria kufanya uchunguzi wa kina. Hatutakuwa na raha hadi aliyempiga risasi afikishwe mahakamani. "
Kamati ya Kupambana na Ubaguzi wa Waarabu wa Marekani ilisema, "Tuna sababu ya kuamini kwamba ufyatuaji risasi ulitokea kwa sababu waathiriwa ni Waarabu." Ilitoa wito kwa mamlaka ya Vermont kuchunguza upigaji risasi huo kama uhalifu wa chuki.
Ikulu ya White House ilisema Rais Joe Biden alikuwa amearifiwa kuhusu shambulio hilo.
Bernie Sanders, seneta huru wa Vermont na mgombea urais wa zamani, alitaja shambulio hilo "la kushtua na kuhuzunisha sana," na kuongeza, "Chuki haina nafasi hapa, au popote."
Ufyatulianaji wa risasi umekuja wakati mashirika ya kutetea haki za kiraia yameonya juu ya kuongezeka kwa uhalifu wa chuki dhidi ya Wamarekani Waarabu na Waislamu.
Mwezi uliopita, mvulana mwenye umri wa miaka sita Mpalestina na Marekani aliuawa kwa kuchomwa kisu huko Illinois, huku mama yake akijeruhiwa. Mshukiwa mwenye umri wa miaka 71 amekana mashtaka.