Mahakama Pakistan yamkuta Imran Khan na hatia katika kesi ya ufisadi

Mahakama Pakistan yamkuta Imran Khan na hatia katika kesi ya ufisadi

Serikali imetuma wanajeshi kukabiliana na waandamanaji wanaopinga kukamatwa kwa Imran Khan
Imran Khan akutwa na hatia katika kesi ya ufisadi dhidi yake: TRT World

Mahakama nchini Pakistan imemkuta aliyekuwa Waziri Mkuu Imran Khan na hatia katika kesi iliyomkabili ya ufisadi.

Khan alishutumiwa kwa kosa la kuuza zawadi za serikali kinyume cha sheria na kosa lingine la kutowasilisha zawadi za serikali kwa Toshakhana, hazina ya taifa inayopokea zawadi zozote zinazotolewa kwa serikali.

Khan amerudishwa rumande kwa muda wa siku nne akisubiri uamuzi wa mahakama juu ya hukumu yake.

imran Khan, aliyeondolewa kama waziri mkuu wa Pakistan Picha : Reuters

Wakati huo huo serikali imetuma wanajeshi kukabiliana na waandamanaji wanaopinga kukamatwa kwa Khan.

Kuanzia Jumanne, alipokamatwa waziri huyo mkuu wa zamani nje ya mahakama kuu, ghasia ziliibuka kati ya wafuasi wake na polisi na kusababisha kifo cha mtu mmoja na kujeruhiwa zaidi ya watu 12, wakiwemo polisi 6.

Waziri wa Usalama wa Ndani wa Pakistan Rana Sanaullah Khan, amesema kuwa hawata ruhusu ghasia zozote kukabiliana vikali na ghasia zozote kutoka kwa wafuasi

''Tumetoa amri kuwadhibiti wafuasi wa Khan kutumia nguvu zote iwapo watasababisha vurugu za aina yoyote,'' alisema waziri huyo.

Pakistan, waandamanaji wachoma vitu arabarani kulalamikia kukamatwa kwa Imran Khan : Picha TRT World

Duru za polisi zimeelezea kuwa kufikia Jumatano mchana watu 945 wametiwa nguvuni kuhusiana na ghasia hizo, ambazo zimesababisha kuchomwa kwa magari 14 ya polisi na uharibifu na wizi katika zaidi ya majengo 14 za seriikali.

Kesi ya Imran Khan imesikilizwa katika 'nyumba salama' badala ya kupelekwa mahakamani.

''Khan hakupelekwa mahakamani kama tahadhari kwa usalama wake na wa serikali. Serikai inachukua tahadhari zote hizi kulinda mali za umma na maeneo muhimu,'' amesema Ihsan Iqbal, Waziri wa Mipango wa Pakistan.

Khan, 70, aliondolewa madarakani mwezi Aprili 2022, kupitia kura ya Imani bungeni na tangu wakati huo amekuwa akisukuma kufanywa uchaguzi wa mapema.

Chama cha waziri mkuu huyo wa zamani, Tehreek-e-Insaf (PTI) kinadai kuwa kesi hizi ni njama za kutaka kumzuia bwana Khan kushiriki uchauzi uliopangwa mwezi Novemba mwaka huu.

TRT Afrika