Mamlaka imelaumu utekaji nyara huo kwa kitengo cha ELN na wameanzisha msako mkubwa wa kumtafuta babake Diaz, Luis Manuel Diaz. Picha Getty

Mkuu wa kundi la wapiganaji la ELN nchini Colombia amekiri kuwa shirika hilo lilifanya "kosa" lilipomteka nyara baba yake mchezaji wa Liverpool Luis Diaz wiki iliyopita, na kuahidi kufanyia kazi kuachiliwa kwake.

Wazazi wa Diaz walitekwa nyara katika mji wa nyumbani kwao wa Barrancas karibu na mpaka wa Venezuela wiki iliyopita, lakini mama yake aliokolewa saa chache baadaye.

Mamlaka imelaumu utekaji nyara huo kwa kitengo cha ELN na wameanzisha msako mkubwa wa kumtafuta babake Diaz, Luis Manuel Diaz.

"Kuendelea kushikiliwa kwa baba ya Luis Diaz na Northern War Front lilikuwa kosa," kamanda wa ELN Antonio Garcia, aliandika kwenye chaneli yake ya Telegram siku ya Jumamosi.

"Lucho ni ishara ya Colombia - hivyo ndivyo sisi katika ELN tunavyohisi juu yake," aliongeza, akitumia jina la utani la Diaz, 26, ambaye amecheza mechi 11 msimu huu akiwa na Liverpool na kufunga mabao matatu.

Tukio hilo limetishia kuvuruga mazungumzo ya hali ya juu ya amani kati ya kundi la waasi na Rais wa mrengo wa kushoto Gustavo Petro, yanayofanyika wakati wa usitishaji vita wa miezi sita.

Malipo ya kikombozi

Siku ya Jumatano, wapatanishi wa amani wa ELN walikubali kwa wenzao wa serikali kwamba vikosi vya kaskazini vinamshikilia babake Diaz.

Katika chapisho lake la Telegram, Garcia alisema kuwa kamandi kuu ya ELN ilikuwa inasimamia juhudi za kumwachilia babake mwanasoka huyo na aliviagiza vitengo vyake kushirikiana.

"Tunatumai kuwa hali ya utendaji kazi inaweza kutatuliwa, huu ndio mwongozo ambao makamanda wanapaswa kuharakisha kuachiliwa," Garcia alisema.

Vyombo vya habari nchini humo vimechapisha taarifa inayodaiwa kuwa ni ya 'vikosi kutoka Kaskazini', ambapo waasi hao wanaeleza kuwa walimteka nyara babake Diaz ili kulipwa kikombozi na hawakutambua kuwa alikuwa babake nyota huyo wa soka nchini humo.

Taarifa haikuweza kuthibitishwa kwa kujitegemea. Marafiki wawili wa babake Diaz wametunga wimbo wa kutaka aachiliwe. "Inatosha kwa utekaji nyara nchini Colombia," mmoja wa watu hao wawili, Libardo Brito, aliiambia AFP.

TRT Afrika