Rais wa Colombia Gustavo Petro amesema nchi hiyo, ambayo inaripotiwa kuwa muuzaji mkuu wa makaa ya mawe kwa Israeli, itasitisha mauzo hayo kwa Tel Aviv kutokana na mashambulizi yake dhidi ya Gaza.
Petro, kutoka mrengo wa kushoto, alikata uhusiano wa kidiplomasia na Israeli mwezi Mei na amemkosoa vikali Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.
Kupitia mtandao wa kijamii wa X, alisema Jumamosi kwamba mauzo ya makaa ya mawe yatasitishwa "hadi mauaji ya kimbari yakomeshwe," akimaanisha vifo vya Wapalestina katika mzozo huo.
Pia alisema kuwa Bogota itaacha kununua silaha zinazotengenezwa na Israeli, mojawapo ya wasambazaji wakuu wa vikosi vya usalama vya nchi hiyo ya Amerika Kusini.
"Colombia inaamini kwamba operesheni za kijeshi dhidi ya watu wa Palestina zinawakilisha uvunjaji wa kanuni ya sheria ya kimataifa," waraka huo ulisema.
Muuzaji mkuu wa makaa ya mawe kwa Israeli
Kulingana na Jarida la Usafirishaji la Marekani, Colombia ndiyo muuzaji mkuu wa makaa ya mawe kwa Israeli, ikiwakilisha zaidi ya nusu ya uagizaji wake.
Israeli inategemea makaa ya mawe kwa asilimia 20 ya uzalishaji wake wa umeme, lakini hiyo inatarajiwa kushuka hadi asilimia 3, na ina vyanzo vingine vya makaa ya mawe, jarida hilo lilisema.
Chama cha kibinafsi cha uchimbaji madini nchini Colombia kimesema marufuku hiyo itakiuka makubaliano ya kimataifa na kuweka imani ya soko na uwekezaji wa kigeni hatarini.
Colombia ni nchi ya tano kwa uzalishaji wa makaa ya mawe duniani, huku Drummond na Glencore zikiwa miongoni mwa wachimbaji wake wakuu.
Nchi ya Colombia ilituma tani milioni 56.7 za makaa ya mawe nje ya nchi mwaka jana, ikiwa ni pamoja na tani milioni 3 kwa Israeli, karibu asilimia 5.4 ya mauzo ya nje, kulingana na data ya serikali ya nchi hio.