Na David Schultz
Tunapofikiria ushindi wa Donald Trump na kupoteza kwa Kamala Harris katika uchaguzi wa rais wa Merika wa 2024, swali ni, nini kilifanyika? Na kwa nini?
Kuna sababu za kimuundo za muda mrefu zinazoelezea kupaa kwa Trump na nadharia ya ''Trumpism'', pamoja na masuala ya muda mfupi ambayo yanabadilisha muundo wa wapiga kura wa Marekani.
Wanasayansi wa kisiasa kama vile Walter Dean Burnham wamezungumza kuhusu dhana ya uchaguzi muhimu na marekebisho katika siasa za Marekani.
Katika nyakati za mara kwa mara katika historia ya Marekani, uchaguzi ni muhimu sana na unaobainisha usawa wa kisiasa.
Wanazalisha miungano mipya ya uongozi na miunganisho ya upigaji kura miongoni mwa wapiga kura.
Nchini Marekani, nchi hiyo imeona kufichuliwa taratibu kwa kile ambacho hapo awali kilikuwa Muungano wa New Deal wa miaka ya 1930, muungano wa Chama cha Kidemokrasia unaojumuisha vyama vya wafanyakazi, walio wachache, Wakatoliki, Wayahudi na wakulima.
Urekebishaji wa kisiasaMuungano huo ulijengwa upya katika miaka ya 1960 na 1970, na kuubadilisha baada ya Sheria ya Haki za Kiraia ya 1964, Sheria ya Haki za Kupiga Kura ya 1965, na uamuzi wa Mahakama Kuu ya 1973 Roe v. Wade kuwa chama cha haki za wachache na utoaji mimba.
Mizizi ya kitamaduni ya ''Trumpism'' inaanzia hapa, na Richard Nixon wa kwanza mnamo 1968 na kisha Ronald Reagan mnamo 1980 akigombea kama wagombeaji wanaopinga mapinduzi ya kitamaduni ya 1960s.
Walitoa wito kwa wazungu waliosahaulika wa tabaka la kati na wafanyikazi waliohisi kupuuzwa na mabadiliko katika jamii.
Zaidi ya hayo, katika miaka ya 1970 na 1980, uchumi wa Marekani, ambao ulikuwa umejengwa karibu na viwanda na wafanyakazi, ulivurugika. Ajira zaidi ya milioni 37 za viwanda zilitoweka, zingine kwa sababu ya uuzwaji wa nje, zingine kwa sababu ya teknolojia.
Wafanyakazi, wale wasio na shahada ya chuo kikuu, au hata shahada ya shule ya upili, ambao hapo awali waliweza kufaulu kiuchumi na kustawi sasa ghafla walijiona kuwa wahasiri katika uchumi ambao ulikuwa unazidi kuwa wa teknolojia ya juu na unaozingatia huduma.
Ukosefu wa usawa wa kiuchumi sasa hivi ulilipuka hadi kufikia kiwango kikubwa, lakini Wanademokrasia waliacha kushughulikia suala hili.
Chama cha Democratic chini ya marais Bill Clinton na hatimaye Barack Obama walishindwa kuzungumza na watu hawa. Walichagua kuunda upya Chama cha Kidemokrasia karibu na wasomi waliosoma chuo kikuu, wenye uwezo wa kufanya vyema kiuchumi, wakiwa na wasiwasi mdogo kuhusu kulipa rehani na zaidi kuhusu siasa za utambulisho.
Wakati mdororo wa uchumi wa 2008 ulipotokea, Obama alifanya makosa ya kimkakati. Yeye na utawala wake waliamua kuziokoa benki na sio wamiliki wa nyumba na tabaka la wafanyikazi. Na hivyo, mnamo 2016 Donald Trump alijitokeza.
Kupata ijna kwa Trump
Trump alidai kuwa Wanademokrasia hawakujali tabaka la wafanyikazi weupe, na Chama cha Republican vivyo hivyo.
Trump alizungumza na hofu na wasiwasi wa kiuchumi wa Wamarekani wengi ambao walihisi kupuuzwa. Ndiyo, ujumbe wake ulionekana sana kama chuki dhidi ya wageni na ubaguzi wa rangi, lakini uligusa maadili ya Wamarekani wengi huku akijiweka kama mbadala wa siasa za kawaida.
Ubaguzi wa kijinsia kwa kiwango fulani kilimuangusha Hillary Clinton mnamo 2016, lakini alikuwa na mapungufu yake ya kisiasa, na hatimaye kuendesha kampeni iliyojaa makosa yenye ujumbe na mkakati mbaya.
Trump alishindwa tu mnamo 2020 labda kwa sababu ya kushughulikia vibaya janga hili, na mahitaji ya utulivu wa kisiasa.
Wanademokrasia walikusanya tena muungano wa kisiasa unaofifia wa chama chao nyuma ya Rais Joe Biden na kumshinda Trump. Lakini ikiwa kura 43,000 za majimbo yasioegemea upande wowote ya Arizona, Georgia, na Wisconsin, Trump angeshinda tena.
Kufikia 2024, mapungufu ya Biden na Chama cha Kidemokrasia yalikuwa dhahiri. Biden alikuwa rais dhaifu kwa sababu ya umri wake na mapungufu yake ya kiakili.
Zaidi ya hayo, usawa wa kimuundo wa uchumi wa Marekani ambao ulikuwa ukijengwa kwa miaka 50 uliendelea.
Wengi waliona katika miaka minne iliyopita bei ya maziwa, mkate, mayai na mahitaji mengine ikipanda, na walikuwa wanapata shida kujidumu.
Ingawa matajiri walikuwa wakitangaza kwamba Wall Street na uchumi wa Marekani ulikuwa unaendelea vizuri, watu wa kila siku wanaoishi kwenye mitaa yao walikuwa na shida kulipa kodi au rehani.
Wakati huo huo, mabadiliko ya watu wa rangi na idadi ya watu katika baadhi ya maeneo yalifanya baadhi ya watu wahisi wasiwasi, na itikadi kali za vita vya kitamaduni viliochochewa na vyombo vya habari uliimarisha hisia hizo.
Makosa ya Biden yalipodhihirika na Harris akachukua nafasi yake, hakuweza kurekebisha shida za kimsingi ambazo yeye na Chama cha Kidemokrasia walikuwa wameweka mbele yake.
Labda alikuwa mgombea asiye sahihi na ujumbe na mkakati usio sahihi, lakini labda hakuna mgombeaji wa Chama cha Demokrasia ambaye angeshinda uchaguzi huu.
Mkakati wa kukinaisha
Kamala Harris, hakuwa na ushawishi wa kukinaisha kwa nini anapaswa kuwa rais, isipokuwa labda kusema kwamba Trump alikuwa mbaya.
Yeye na Wanademokrasia walitegemea sana uavyaji mimba na haki za uzazi kama kipaumbele na waliendesha kampeni uliojaaa utamaduni.
Ubaguzi wa kijinsia na ubaguzi wa rangi huenda ukaeleza hasara yake, lakini zaidi yalitokea.
Matokeo ya uchaguzi yanaonyesha Marekani imehamia upande wa kulia. Hata wanawake, ingawa walikuwa na wasiwasi juu ya utoaji mimba, waliondoka kwake kwa sababu ya masuala ya kiuchumi.
Kampeni ya Trump inaogemea upande wa wanaume kwa hakika ilimsaidia kuwaleta wapiga kura wanaume upande wake, lakini msingi wa ujumbe wake ulikuwa ule ambao ulivutia jamii mbalimbali kuhusu watu waliokuwa bado wanasahaulika.
Ingawa Harris hakuwahi kugombea waziwazi kama mgombeaji wa rangi mchanganyiko wa kike, kiini cha kampeni yake kilikuwa historia yake, ambayo ilikuwa na ujumbe wa idadi ya watu (demographia).
Lakini demografia sio kila kitu. Nguvu za msingi za kiuchumi na hisia ya kutengwa na jamii ni vielelezo muhimu vya tabia ya kupiga kura.
Kilichosababisha kushindwa kwa uchaguzi huu si matokeo ya muda mfupi, bali ni urekebishaji wa kimuundo muhimu wa muda mrefu wa wapiga kura. Wanademokrasia wamepoteza tabaka la wafanyikazi, wakiwemo wapiga kura vijana na wanawake wengi ambao wanaendelea kuhangaikia hali yao ya kiuchumi.
Bado haijafahamika iwapo Warepublican wanaweza pia kushikilia sehemu hii ya wapiga kura, kulingana na jinsi utawala wa Trump utakavyoshughulikia wasiwasi wao katika miaka ijayo.
Lakini hadi wakati ambapo Wanademokrasia watajifunza jinsi ya kuzungumza na watu hawa, na kuwavutia, wataendelea kupoteza. Labda sio sana, lakini bado, watapoteza.
Mwandishi, David Schultz ni profesa mashuhuri wa Chuo Kikuu cha Hamline wa Sayansi ya Siasa, Mafunzo ya Sheria, na Mafunzo ya Mazingira huko Saint Paul, Minnesota. Yeye ndiye mwandishi wa vitabu zaidi ya 45 na nakala 200.
Kanusho: Maoni yaliyotolewa na mwandishi hayawakilishi lazima maoni, mitazamo na sera za uhariri za TRT Afrika.