Kimbunga kikali kimeupiga mji wa Texas Panhandle wa Perryton siku ya Alhamisi, na kuua watu watatu, kujeruhi na kusababisha uharibifu mkubwa huku muendelezo wa dhoruba kali ukipitia majimbo ya Kusini.
Mamlaka ya Kitaifa ya Hali ya Hewa huko Amarillo ilithibitisha kwamba kimbunga kilipiga eneo hilo muda mfupi baada ya saa kumi na moja jioni siku ya alhamisi. Pia maafisa wa eneo hilo walisema kwamba watu wawili walipotea.
Mkuu wa Zimamoto wa Perryton Paul Dutcher alisema angalau mtu mmoja aliuawa katika eneo lenye nyumba zinazo hamishika ambapo nyumba hiyo ilipata "pigo moja kwa moja".
Dutcher alisema angalau trela 30 zilibomolewa au kuharibiwa kabisa.
Nyumba zinazo hamishika zilibomolewa na malori yaliyokuwa yamevunjwa vioo yalibamizwa dhidi ya vifusi katika maeneo ya makazi.
Takriban sehemu mbili za biashara ziliharibiwa sana, ikijumuisha duka la vifaa vya ofisi, duka la maua na saluni ya nywele kando ya barabara kuu ya jiji.
Idara husika ilisema itaweka amri ya kutotoka nje usiku hadi asubuhi Ijumaa kwa sababu ya njia za umeme kukatika na hatari nyinginezo ambazo huenda zisionekane gizani.