Mvua kubwa za monsuni zimesababisha maeneo kadhaa ya New Delhi kujaa maji mengi, huku kukiwa na tahadhari ya upungufu wa maji baada ya Mto Yamuna kuvunja kingo zake.
Tangu msimu wa monsuni uanze tarehe 1 Juni, Delhi imepokea mvua zaidi ya asilimia 113 ya wastani, kwa mujibu wa Idara ya Hali ya Hewa ya India, na mvua katika majimbo ya milima kaskazini mwa nchi imesababisha mafuriko katika mto huo.
Video zinaonyesha barabara zilizozama katika eneo la katikati mwa mji, ambapo kuna ofisi za serikali na kampuni binafsi, na maji yamefikia nusu ya magari yaliyopakiwa.
Picha nyingine zinaonyesha barabara karibu na ngome ya kihistoria ya Red Fort ikiwa chini ya maji.
Mji wenye watu milioni 20 umetoa amri ya kufunga shule zote, vyuo na vyuo vikuu hadi Jumapili na imezuia wafanyakazi wasio muhimu serikalini wasifike kazini, alisema Mkuu wa Mkoa wa Delhi, Arvind Kejriwal, Alhamisi.