Mtandao wa wanaharakati wa hali ya hewa (Climate Action Network, CAN ) unalaani uvamizi wa Israel dhidi ya Gaza na unataka usitishaji wa vita mara moja na wa kudumu.
CAN ni mtandao wa mashirika ya kutetea mazingira, katika nchi zaidi ya 130.
Wakati huo huo, CAN inaitaka Israeli kuwajibishwa kwa uhalifu wa kivita inaofanya.
"Tunatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua za haraka na madhubuti ili kuhakikisha kuwa Israel inatii hatua zote za tahadhari zinazohitajika na Mahakama ya Kimataifa ya Haki," limesema Shirika hilo katika taarifa yake.
CAN inazitaka nchi hizo zinazoiunga mkono Israeli kupitia usambazaji wa silaha kufuata sheria za kimataifa za kuzuia mauaji ya halaiki.
"Kwa hivyo CAN inasisitiza kuwekwa vikwazo vya kimataifa vya silaha dhidi ya Israeli na tutatoa shinikizo kwa hili," taarifa yake imeongezea.
Shirika hili limesisitiza kuwa kukomeshwa kwa uvamizi wa Palestina kwa mujibu wa maazimio ya Umoja wa Mataifa ni sharti la kuhakikisha suluhu la kudumu.
"Wapalestina wanakabiliwa na kizuizi kamili, njaa, magonjwa, uhamishaji wa lazima na uharibifu wa miundombinu yote. Hatutanyamaza mbele ya mauaji ya kimbari yanayotokea," mtandao huo umeongezea.
Wanachama wa Climate Action Network CAN walipaza sauti zao kuunga mkono Palestina wakati wa mkutano wa COP 28 huko Dubai uliofanyika kati ya Novemba 30, 2023 hadi Desemba 13, 2023.