Risasi zilifyatuliwa wakati wa hotuba ya Donald Trump, katika tukio ambalo wachunguzi wanachukulia kama jaribio linalowezekana la kumuua rais huyo wa zamani.
Pamoja na Abraham Lincoln na JFK, hii hapa ni baadhi ya mifano mashuhuri ya ufyatuaji risasi unaohusisha marais wa Marekani au wagombea urais:
Ronald Reagan (1981)
Rais Reagan alipigwa risasi na kujeruhiwa vibaya alipokuwa akitoka kwenye hafla katika hoteli ya Hilton mjini Washington. Mshambuliaji alikuwa John Hinckley Jr, ambaye aliruhusiwa kuachiliwa bila masharti mnamo 2022.
Reagan alikaa siku kumi na mbili hospitalini. Tukio hilo liliongeza umaarufu wa Reagan, kwani alionyesha ucheshi na ujasiri wakati wa kupona kwake.
Gerald Ford (1975)
Rais Gerald Ford aliponea bila kujeruhiwa katika majaribio mawili tofauti ya mauaji ya wanawake mnamo Septemba 1975, huko California na ndani ya muda wa siku 17 tu.
George Wallace (1972)
Akiwa katika kampeni za kuteuliwa kuwa mgombea wa kiti cha urais wa Demokrats Wallace alipigwa risasi nne na kupooza maisha yake yote katika jumba la maduka huko Laurel, Maryland.
Jaribio la kumuua Wallace, ambaye alijulikana kwa maoni yake ya ubaguzi na siasa za kuwavutia walio wengi, ilionyesha mivutano ya kisiasa inayoendelea nchini Marekani na uwezekano wa vurugu za nyumbani katika enzi ya Vita vya Vietnam.
Robert F. Kennedy (1968)
Kakake Rais John F. Kennedy Robert, ambaye alikuwa anawania uteuzi wa urais wa chama cha Democratic, alipigwa risasi na kuuawa katika hoteli ya Ambassador mjini Los Angeles, California.
Mauaji hayo yalikuwa na athari kubwa katika kinyang'anyiro cha urais wa 1968 na yalitokea miezi miwili tu baada ya mauaji ya kiongozi wa haki za kiraia Martin Luther King Jr, na kuongeza msukosuko wa kisiasa wa mwishoni mwa miaka ya 1960.
John F. Kennedy (1963)
Akiwa kwenye msafara wake wa magari na mkewe Jackie, Rais John F. Kennedy aliuawa huko Dallas, Texas na Lee Harvey Oswald.
Tume ya Warren iliyochunguza mauaji hayo ilihitimisha mwaka wa 1964 kwamba Lee Harvey Oswald, baharia wa zamani aliyeishi katika Muungano wa Sovieti, alikuwa ametenda peke yake.
Wamarekani wengi wanaamini kuwa kifo cha JFK kilianza kipindi cha vurugu zaidi katika siasa za Marekani na jamii, huku Vita vya Vietnam vikiendelea na mapambano ya haki za kiraia kama vichocheo.
Franklin D. Roosevelt (1933)
Akiwa rais mteule, Franklin D. Roosevelt alikuwa mlengwa wa jaribio la mauaji huko Miami, Florida.
Hakujeruhiwa, lakini Meya wa Chicago Anton Cermak aliuawa katika shambulio hilo.
Theodore Roosevelt (1912)
Kama Trump, Teddy Roosevelt alikuwa akigombea Ikulu ya White House kama rais wa zamani alipopigwa risasi huko Milwaukee, Wisconsin.
Risasi hiyo, iliyobaki kifuani mwake maisha yake yote. Risasi ilipunguzwa kasi na hotuba iliyokunjwa ya kurasa 50 na glasi ya chuma kwenye mfuko wake wa kifuani.
Maarufu, Roosevelt aliamua kutoa hotuba yake iliyopangwa licha ya kupigwa risasi.
William McKinley (1901)
Rais William McKinley alipigwa risasi na kuuawa na mwana vuguvugu Leon Czolgosz huko Buffalo, New York.
Abraham Lincoln (1865)
Abraham Lincoln aliuawa na John Wilkes Booth, mwigizaji mashuhuri na mshiriki wa Muungano wakati akitazama mchezo uitwao "Our American Cousin" kwenye ukumbi wa Ford's Theatre huko Washington.
Mashambulizi ya Booth, siku chache baada ya Muungano wa kibaguzi wa Confederate kusalimu Vita vya wenyewe kwa wenyewe, ilikuwa sehemu ya njama kubwa iliyojumuisha majaribio ya kumuua Makamu wa Rais Andrew Johnson na Waziri wa mambo ya nje William Seward.