Kundi la Wapalestina la Hamas limewakabidhi mateka watano wa Israel kwa Msalaba Mwekundu katika maeneo mawili yaliyotengwa huko Gaza chini ya makubaliano ya kusitisha mapigano ya Gaza, huku ikitarajiwa kukabidhi mateka wa sita hivi karibuni.
Mabadilishano ya mateka kati ya Hamas na Israel siku ya Jumamosi ni mabadilishano ya saba katika awamu ya kwanza ya makubaliano ya kusitisha mapigano Gaza.
Kundi la Wapalestina liliteua maeneo mawili ya makabidhiano: moja huko Rafah, sehemu ya kusini ya eneo lililozingirwa, na lingine huko Nuseirat, katikati mwa Gaza.
Huko Rafah, eneo lililoteuliwa lilikuwa chini ya kilomita moja kutoka maeneo ya jeshi la Israel kusini mwa mji huo.
Eneo hilo lilishuhudia mkusanyiko mkubwa wa Wapalestina.
Mateka wawili wa Israeli, Tal Shoham na Avera Mengistu, walikabidhiwa katika eneo hili.
Ubaguzi wa rangi
Vile vile, huko Nuseirat, umati wa Wapalestina walikusanyika katika eneo lililotengwa, wakitarajia kukabidhiwa kwa mateka wengine wanne.
Mateka Eliya Cohen, Omer Shem-Tov, na Omer Wenkert waliachiliwa huru huko Nuseirat.
Mateka wa sita, Hesham al-Sayed mwenye umri wa miaka 36, pia anatazamiwa kuachiliwa hivi karibuni, ikiripotiwa bila sherehe katika Jiji la Gaza.
Avera Mengistu na Hisham Al-Sayed, mateka wawili walioachiliwa leo wameshikiliwa Gaza tangu 2014 na 2015 mtawalia.
Hamas imekuwa ikishinikiza kubadilishana wafungwa na Israel kwa Mengistu na Al-Sayed kwa miaka mingi, lakini Tel Aviv mara kwa mara imekuwa ikichukia wazo hilo.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu yameikashifu Israel mara kadhaa kwa kubagua uhuru wa mateka hao wawili, wakiishutumu Israel kwa ubaguzi wa rangi.
Kwa kubadilishana, Israel inatazamiwa kuwaachilia wafungwa 602 wa Kipalestina, wakiwemo 50 wanaotumikia vifungo vya maisha na 60 wenye vifungo vya muda mrefu.
Wafungwa 47 ambao walikamatwa tena baada ya kuachiliwa huru katika mkataba wa Shalit wa 2011 pia wataachiliwa huru pamoja na wafungwa 445 kutoka Gaza ambao walizuiliwa baada ya Oktoba 7, 2023.