Rais wa Marekani Joe Biden ameonya kwamba uamuzi muhimu wa Mahakama ya Juu wa Marekani kuhusu kinga ya rais unaweka "mfano hatari" ambao Donald Trump angeutumia akichaguliwa mwezi Novemba.
"Kwa madhumuni yote ya kiutendaji, uamuzi wa leo kwa hakika unamaanisha kuwa hakuna kikomo kwa kile rais anaweza kufanya. Hii ni kanuni mpya kimsingi, na ni mfano wa hatari," Biden alisema katika hotuba yake katika Ikulu ya White House siku ya Jumatatu.
"Watu wa Amerika lazima waamue ikiwa wanataka kukabidhi ... kwa mara nyingine, urais kwa Donald Trump, sasa akijua atakuwa na ujasiri zaidi wa kufanya chochote anachotaka, wakati wowote anapotaka kufanya," aliongeza.
Katika uamuzi wa 6-3, Mahakama ya Juu iliamua kwamba Trump anaweza kudai kinga dhidi ya mashtaka, uwezekano wa kuchelewesha kesi yake ya Januari 6.
"Hakuna wafalme Marekani. Kila mmoja wetu ni sawa mbele ya sheria. Hakuna, hakuna aliye juu ya sheria, hata rais wa Marekani," Biden alisema.
Mahakama ya Juu haikutupilia mbali - kama Trump alivyotaka - shtaka linalodai alipanga njama kinyume cha sheria kung'ang'ania mamlaka baada ya kushindwa na Biden.
Lakini uamuzi huo bado ni sawa na ushindi mkubwa kwa mteule wa urais wa chama cha Republican anayetarajiwa, ambaye mkakati wake wa kisheria umelenga kuchelewesha kesi hadi baada ya uchaguzi.
Trump alichapisha kwa herufi kubwa zote kwenye mtandao wake wa kijamii muda mfupi baada ya uamuzi huo kutolewa: “USHINDI MKUBWA KWA KATIBA YETU NA DEMOKRASIA NAJIVUNIA KUWA MMAREKANI!”
Wakati wa kesi hiyo ni muhimu kwa sababu ikiwa Trump atamshinda Biden, anaweza kuteua mwanasheria mkuu ambaye angetaka kufutwa kwa kesi hii na mashtaka mengine ya shirikisho anayokabili.
Au pengine Trump anaweza kuamuru msamaha wake mwenyewe.