Kampuni ya saruji Lafarge sasa imegundulika kuwa inafadhili vitendo vya kigaidi, Rais wa Turkiye Recep Tayyip Erdogan amesema.
“Niliposema kuwa Lafarge inafadhili makundi ya kigaidi kaskazini mwa Syria, watu wengi kutoka Ufaransa hawakunielewa. Nilimweleza Macron. Sasa Wabunge wa Ufaransa wanataka kufahamu taarifa kuhusu akaunti ya kampuni hiyo.” Rais Erdogan aliwaambia mawaziri wa habari katika kongamano la muungano wa waislamu jijini Instanbul siku ya Ijumaa.
“Sasa hivi Lafarge imekuwa gumzo kubwa nchini Ufaransa baada ya kugundulika kuwa ni kweli inafadhili ugaidi.” Aliongeza Erdogan.
Faini kubwa
Kampuni ya Lafarge ilipigwa faini kubwa ya dola milioni 778 na mahakama moja nchini Marekani kwa kosa la kufadhili makundi ya kigaidi nchini Syria kati ya 2013-2014, likiwemo kundi la Daesh.
Rais Erdogan alisema licha ya kuwa Turkiye ndiyo nchi pekee inayopigana na kundi la Daesh, watu wengi wanailimbikizia madai mengi ya uongo.
“Ni Dhahiri sasa kuwa waliotudharau miaka ya jana kumbe walikuwa wakifanya biashara na magaidi, kwa kuwatumia mamilioni ya pesa katika kipindi hicho.” Alisema Erdogan.