Mahojiano na Erdogan/ Picha AA

Uturuki imeweza kubana udhibiti wa Abu al Qurayshi, anayedaiwa kuwa kiongozi wa kundi la kigaidi la Daesh, katika operesheni nchini Syria, rais Recep Tayyip Erdogan ametangaza.

‘’Shirika la kitaifa la intelijensia, MIT, limekuwa likimfuatilia kiongozi huyo wa Daesh, kwa jina la Abu Hussain al Qurayshi kwa muda mrefu.’’ Erdogan alisema katika mahojiano ya moja kwa moja na televisheni ya kitaifa ya Uturuki, TRT, siku ya Jumapili.

‘’Hii ndio mara ya kwanza nazungumzia hili hapa. Gaidi huyo alidhibitiwa katika operesheni iliyofanywa na MIT hapo jana.‘’ Aliongeza.

‘’Tutaendelea kukabiliana na mashirika yote ya kigaidi bila kuchagua’’ aliongeza.

Mnamo mwaka 2013 Uturuki ilikuwa nchi ya kwanza kulitangaza kundi la Daesh kuwa la kigaidi.

Tangu wakati huo Uturuki imeshambuliwa na kundi hilo la kigaidi mara kadhaa, huku zaidi ya watu 300 wakiuawa, wengine mamia kujeruhiwa katika visa kumi vya ulipuaji wa kujitoa mhanga, mashambulio ya bomu saba na mashambulio manne ya risasi.

Katika kujibu, Uturuki ilianzisha operesheni ya kukabiliana na magaidi ndani ya nchi na nje, ili kuzuia mashambulio zaidi.

‘Chuki dhidi ya uislamu waongezeka nchi za magharibi’

Erdogan amesema kuwa chuki dhidi ya waislamu na ubaguzi umeendelea kusambaa katika mataifa ya magharibi ‘kama saratani’ akiongeza kuwa ‘Mataifa ya magharibi hawajaonesha juhudi zozote za kukabiliana na tishio hili.’

Matamshi ya chuki na mashambulio yanayolenga waislamu na misikiti imeendela kuongezeka katika nchi hizo, alisema.

‘Matendo ya kuchukiza, kama vile kuchoma misikiti na nakala za Quran, yameongezeka sana… Tutachukua hatua zote kuhakikisha maisha yanalindwa pamoja na mali za raia wetu,’ aliongeza Erdogan.

Katika miezi ya hivi karibuni kumeongezeka visa vya watu kuchoma nakala za Quran, au jaribio la kufanya hivyo, na watu wanaohusishwa na makundi ya wachochezi dhidi ya waislamu, kaskazini mwa Ulaya na nchi za Nordic.

Na kuhusu kundi la ki-Nazi la National Socialist Underground Group (NSU), Erdogan amesema kuwa Uturuki itaendelea kuwafuatilia kwa makini.

‘Ikihitajika, basi tutawafungulia kila aina ya mashtaka katika mahakama za kimataifa, ikiwemo kutaka fidia za kifedha hadi kesi zisizo na fidia, almuradi tupate matokeo bora,’ aliongeza.

Kundi hilo la kigaidi la mrengo wa kulia NSU liliwaua waturuki wanane wahamiaji, raia mmoja wa Ugiriki na polisi mmoja wa Ujerumani kati ya mwaka wa 2000 na 2007 lakini kesi hizo hazijatatuliwa hadi leo.

TRT Afrika