Kamusi maarufu ya Kiingereza ya Oxford./Picha: Getty

Kamusi maarufu ya Kiingereza ya Oxford imeongeza maneno mapya matatu kutoka lugha ya Kiswahili.

Maneno hayo ni "Panya Route," "Kitu Kidogo" na "Rolex," ambayo yamejizoelea umaarufu katika ukanda wa Afrika Mashariki, hususani katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda.

Neno Panya Route ni maarufu sana nchini Kenya na Tanzania likimaanisha ‘njia za mkato au za kimagendo', wakati ukiwa nchini Kenya na ukisikia mtu ametamka Kitu kidogo , basi elewa kuwa hizo ni pesa zinazotolewa au kukubaliwa kama kishawishi au hongo.

Rolex chakula maarufu nchini Uganda kinachopikwa kutoka na mchanganyiko wa mayai, mboga mboga na chapati./ Picha na wengine.

Na ukienda Uganda, Rolex ni chakula maarufu kinachopikwa kwa kutumia mayai na mboga zilizofungwa ndani ya chapati, ambacho huuzwa na wachuuzi wa mitaani na kuliwa kama chakula au kitafunio.

Hii si mara ya kwanza kwa kamusi ya Kiingereza kuongeza maneno ya Kiswahili. Hapo awali, iliwahi kuongeza maneno kama vile nyama choma, ahsante sana, collabo na sambaza.

TRT Afrika