Kenya imesema inaweza kunasa, kupunguza na kuepuka takriban tani milioni 30 za kaboni kwa mwaka./ Picha : Wizara ya Mazingia Kenya 

Kenya imewataka wadau wanaounda sera za mauzo ya kaboni kuwashirikisha wananchi wa kawaida Afrika kama njia muafaka zaidi ya ufikiaji malengo ya kupunguza uzito wa kaboni katika mazingira.

''Ni vipi tunaweza kumvutia yule mkulima wa kawaida wa majani chai, kwa mfano, kuelewa na kuchangia katika mjadala huu juu ya mauzo ya kaboni?'' aliuliza waziri mwandamizi Musalia Mudavadi. '' Mkulima anatakiwa ajue anapozalisha majani yake n akuuza, anaweza kufaidi dola mbili tatu juu kutokana na mauzo ya kaboni,'' aliongeza Waziri Mudavadi.

Waziri mwandamizi Musalia Mudavadi alikuwa akizungumza alipofungua warsha ya siku mbili jijini nairobi, iliyowaleta pamoja zaidi ya washiriki 200, wakiwemo maafisa wa serikali, wafadhili na waendelezaji wa mradi kutoka kote ulimwenguni, ili kubadilishana ujuzi juu ya fursa za soko la kaboni katika bara.

Mudavadi alisema kuwa Kenya inaweza kunasa, kupunguza na kuepuka takriban tani milioni 30 za kaboni kwa mwaka.

"Uwezo wetu ni kutumia hadi dola za Kimarekani milioni 600 kila mwaka ifikapo 2030 kupitia uuzaji wa kaboni zenye ubora wa juu," Mudavadi alisema.

Mudavadi alilalamika kuwa bara Afrika linabeba mzigo mzito kwa tatizo ambalo wahusika wakuu wako nje.

"Mchango wa Afrika katika utoaji wa hewa chafu duniani ni mdogo, lakini bara hili linakabiliwa na hatari kubwa ya mabadiliko ya hali ya hewa. Hata hivyo, hii sio sababu ya kukata tamaa bali ni uwezo na fursa ambayo haijatumiwa,” Mudavadi aliongeza.

Kulingana na Mudavadi, masoko ya kaboni yameibuka kama nyenzo muhimu ya kifedha ambayo inaweza kuchochea hatua ya hali ya hewa kwa kutoa mtiririko wa fedha za kaboni ili kuchochea ukuaji wa kijani.

Kwa upande wake waziri wa mazingira misitu na mabadiliko ya tabia nchi Soipan Tuya amesema kuwa Kenya imeshika mustakbali wa kudhibiti mabadiliko ya tabia nchi kwa uwekezaji mkubwa katika miradi ya kusafisha hewa.

''Kenya ina mgao mkubwa zaidi wa Mfumo Safi wa Maendeleo katika Afrika Mashariki na jumla ya miradi 210 zilizosajiliwa, hasa katika sekta tatu kuu zikiwemo nishati mbadala iliyounganishwa na gridi ya taifa (jotoardhi na upepo kwa zaidi ya 39%), majiko ya kupikia yaliyoboreshwa (40%) na utakaso wa maji (20%),'' alisema Waziri Tuya.

TRT Afrika