Niger Streets calm

Mji mkuu wa Niger ulikuwa shwari siku ya Jumapili, huku raia wakionekana kutotilia maanani tishio la uingiliaji kijeshi wa jumuiya ya kikanda ya Afrika Magharibi, baada ya muda wa mwisho kwa viongozi wa mapinduzi kumrejesha madarakani rais kumalizika.

Katika mitaa ya Niamey kulikuwa na dalili za mara kwa mara za kuunga mkono serikali ya kijeshi, ambayo imeapa kutoachia madaraka kufuatia unyakuzi wa mamlaka wa Julai 26.

Awali shirika la Reuters liliripoti kuwa takriban watu 100 waliweka kambi karibu na kituo cha wanahewa huko Niamey na kuahidi kuunga mkono utawala mpya wa kijeshi ikihitajika.

Hii inaleta sintofahamu miongoni mwa majirani wa nchi hiyo, ambao tangu mapinduzi kufanyika wamekuwa wakitafuta kumrejesha Rais Bazoum madarakani kwa kutoa kila aina ya vitisho ikiwemo kuivamia nchi hiyo kijeshi.

Hatahivyo viongozi wa mapinduzi hayo wameonekana kukaa ngangari na kutishia kuwa watakabiliana na yeyote atakayejaribu kuingilia nchi hiyo kijeshi.

Viongozi hao wamepata kuungwa mkono na baadhi yamataifa jirani Kama vile Mali, Burkina Faso na Chad, ambao wenyewe wako chini ya uongozi wa kijeshi ulionyakua madaraka kwa nguvu.

ECOWAS pia ilipata pigo kufuatia kukataliwa ombi la la kutuma jeshi Niger , na bunge la Senate la Nigeria.

Maseneta hao, wamesema kuwa japo wanapinga vikali mapinduzi ya kijeshi Niger, wanapendekeza kufuatwa mbinu zingine za kidiplomasia wakihofia muingilio wa kijeshi utachochea machafuko zaidi katika eneo hilo la Afrika Magharibi.

haya ni mapinduzi ya 7 katika eneo hilo la Afrika Magharibi na kati katika kipindi cha miaka mitatu tu.

TRT Afrika
Reuters