Kihistoria, Waafrika wamekuwa wakiongoza katika kuwasilisha maomba ya viza ya Shengen. Licha ya kuwa na idadi kubwa ya maombi, lakini pia, maombi yao yanaongoza kukataliwa, huku Algeria ikiwa mstari wa mbele kunyimwa viza ya Shengen.
Idadi kubwa ya kukataliwa kwa maombi ya viza kumesababisha raia kutoka Afrika kutumia fedha nyingi zaidi kila mwaka, katika malipo ya ada yanayojulikana kama “malipo yasiyorudishwa” yakinufaisha nchi za Umoja wa Ulaya, Shengen, hayo ni kwa mujibu wa jarida la News.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Takwimu za Viza za Shengen, mwaka 2023, maombi 704,000 yamekataliwa kutoka raia wa mataifa ya Afrika.
Hii ina maana kwamba, kiasi cha Yuro milioni 56.3 kimepotea, ikizingatiwa kwamba, ada ya maombi ya viza hairudishwi.
Raia kutoka nchi ya Algeria walikuwa ni waombaji wakubwa wa Viza ya Schengen mwaka 2023.
Algeria inawakilisha asilimia 10.18 ya maombi yaliyokataliwa mwaka 2023.
Kundi hili la waombaji linaathirika zaidi kwa sababu ndio linaloongoza kwa kuwasilisha maombi ya viza na wanaathirika kiuchumi pindi wanapowasilisha maombi yao.
Ada ya maombi ya viza ya Schengen inagharimu kiasi cha €80 ambayo ni sawa na thuluthi moja ya mshahara wa kawaida nchini Algeria ambao ni €300.
Kwa upande wake, mwaka 2023, kumekuwa na jumla ya maombi ya viza 136,367 kutoka Morocco, hii ikiwalisha asilimia 8.3 ya jumla ya maombi ya viza yaliyokataliwa.
Kuhusu gharama, raia wa Morocco walitumia kiasi cha Yuro milioni 10.9 katika maombi ya viza yaliyokataliwa mwaka jana.
Waafrika wanaathirika zaidi na matumizi haya, hasa ikizingatiwa kwamba, wengi kutoka nchi za Afrika, wana kiwango cha chini cha mishahara.
Kwa majumuisho, Afrika inawakilisha asilimia 43.1 ya maombi yote yaliyokataliwa 2023.