| Swahili
MICHEZO
3 dk kusoma
Katibu Mkuu wa CAF ajiuzulu kutokana na shinikizo za ndani na masuala ya utawala bora
Kuondoka kwake kumekuja baada ya wiki kadhaa za shutuma kali kutoka ndani ya uongozi wa CAF, huku wajumbe kadhaa wa Kamati ya Utendaji wakiripotiwa kujiandaa kushinikiza kuondolewa kwake kama asingejiuzulu kwa hiari.
Katibu Mkuu wa CAF ajiuzulu kutokana na shinikizo za ndani na masuala ya utawala bora
Veron Mosengo-Omba CAFVeron Mosengo-Omba ajiuzulu kama Katibu Mkuu wa CAF / Picha : CAF / CAFonline
tokea masaa 8

Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) limeingia katika msukosuko mpya kufuatia kujiuzulu kwa Katibu Mkuu wake, Veron Mosengo-Omba, huku kukiwa na shinikizo la ndani, wasiwasi wa utawala na kuongezeka kwa upinzani juu ya maamuzi ya hivi karibuni ya baraza la bara hilo.

Mosengo-Omba alithibitisha kuwa anajiuzulu kutoka kwa wadhifa wake, na kumaliza muda wake ulioanza Machi 2021, alipoteuliwa kama msimamizi mkuu wa CAF.

Kuondoka kwake kumekuja baada ya wiki kadhaa za shutuma kali kutoka ndani ya uongozi wa CAF, huku wajumbe kadhaa wa Kamati ya Utendaji wakiripotiwa kujiandaa kushinikiza kuondolewa kwake kama asingejiuzulu kwa hiari yake.

Misukosuko na wito wa kuondolewa

Afisa huyo, raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo alikabiliwa na wito wa kumtaka kuondoka madarakani, hasa kutokana na madai kuwa ametimiza muhula wake. Chini ya kanuni za CAF, wafanyikazi wakuu wanapaswa kustaafu wakiwa na umri wa miaka 63, na kuruhusiwa nyongeza moja tu ya miaka mitatu.

Mosengo-Omba, aliyeteuliwa akiwa na umri wa miaka 61, alifikia umri wa kustaafu mwaka 2022 na akaongezewa muda ambao uliisha Oktoba 2025.

Uamuzi wake wa kusalia ofisini zaidi ya kipindi hicho ulizua ukosoaji mkali, huku baadhi ya maafisa wakuu wakielezea msimamo wake kuwa "haramu" na kuhimiza kuchukuliwa hatua mara moja.

Hali hiyo ilifichua wasiwasi mkubwa wa kiutawala ndani ya CAF, huku wakosoaji wakionya kwamba kuruhusu afisa wa juu kuvnja sheria kunadhoofisha uwazi na kunaweza kutilia shaka maamuzi yaliyochukuliwa katika kipindi hicho.

Mzozo wa AFCON unazidisha shinikizo

Shinikizo dhidi ya Mosengo-Omba iliongezeka katika siku za hivi karibuni kufuatia uamuzi tata wa CAF wa kuivua Senegal taji la Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 na kuipa Morocco - hatua iliyozua upinzani mkubwa na pingamizi la kisheria katika Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo.

Muda wa Mosengo-Omba pia ulikumbwa na mizozo ya awali, ikiwa ni pamoja na madai ya ukiukaji wa utawala, malalamiko ya ndani juu ya mazoea ya usimamizi, na uchunguzi wa shughuli za kifedha - ingawa baadhi ya uchunguzi ulifutwa baadaye au haukusababisha kufunguliwa mashtaka.

Uhusiano wake wa karibu na uongozi wa FIFA na ushawishi ndani ya CAF pia umekosolewa na washikadau ambao walitilia shaka uwajibikaji ndani ya shirika hilo.

Licha ya mabishano hayo, Mosengo-Omba alisimamia kipindi cha ukuaji wa kibiashara na mageuzi ya kimuundo ndani ya CAF, ikiwa ni pamoja na juhudi za kupanua mashindano na kuboresha utendaji wa kifedha.

Hata hivyo, muda wake wa takriban miaka mitano - kuanzia Machi 2021 hadi Machi 2026 - unaisha chini ya wingu la upinzani wa ndani na kukosekana kwa utulivu wa kitaasisi, na CAF sasa inakabiliwa na changamoto ya kurejesha imani na kuteua uongozi mpya katika wakati muhimu kwa soka la Afrika.

CHANZO:TRT Afrika Swahili