| Swahili
AFRIKA
2 dk kusoma
Ebola: Mkutano wa India na Afrika wa jijini New Delhi waahirishwa
Mkutano wa India na Afrika ulikuwa umeratibiwa kufanyika wiki ijayo lakini sasa utapangiwa tarehe nyingine.
Ebola: Mkutano wa India na Afrika wa jijini New Delhi waahirishwa
PICHA YA MAKTABA: Kongamano la Nne la India na Afrika lilikuwa limeratibiwa kufanyika Mei 28–31. / REUTERS

India na Umoja wa Afrika wameahirisha mkutano uliokuwa umeratibiwa kufanyika wiki ijayo jijini New Delhi baada ya mlipuko wa Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

"Kwa kuzingatia hali ya afya ilivyo katika bara ... pande zote mbili zimekubaliana kuwa ni bora kuwa na kongamano hilo la Nne la India na Afrika siku nyingine," wizara ya mambo ya nje ya India ilisema.

Mkutano wa India na Afrika ulikuwa umepangwa kufanyika jijini New Delhi kuanzia Mei 28–31.

India imesema iko tayari "kuchangia kwa taasisi ya Afrika ya Kudhibiti Magonjwa (Africa CDC) katika juhudi za kukabiliana na hali ya afya ilivyo".

Hatari siyo kubwa ulimwenguni

Shirika la Afya Duniani limesema Jumatano kuwa hatari ya mlipuko wa Ebola iko juu katika Afrika ya kati lakini siyo kubwa ulimwenguni, likiongeza kuwa virusi huenda vilisambaa kwa miezi kadhaa.

Ebola imesababisha vifo vya watu zaidi ya 15,000 barani Afrika katika kipindi cha nusu karne iliopita.

Mlipuko wa 17 wa Ebola kukumba DRC tayari unasemekana kusababisha vifo 139 kutoka kwa karibu maambukizi 600.

Tahadhari ya kiafya

Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Delhi siku ya Alhamisi ulitoa tahadhari ya kiafya kwa abiria wanaowasili India kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo pamoja na mataifa jirani ya Uganda na Sudan Kusini.

India, ambayo imesisitiza umuhimu wa "kuendeleza ushirikiano wa kuimarisha utayari na kukabiliana na magonjwa kwa watu kote katika bara", inasema itatangaza tarehe nyingine ya mkutano baadaye.

CHANZO:TRT Afrika Swahili