| Swahili
ULIMWENGU
2 dk kusoma
Wanaharakati wa msafara wa Flotilla walioshambuliwa na Israel wapelekwa Uturuki
Zaidi ya wanaharakati 420, wakiwemo raia wa Uturuki 78, wanatarajiwa kuwasili jijini Istanbul kwa ndege ya Shirika la Ndege la Uturuki.
Wanaharakati wa msafara wa Flotilla walioshambuliwa na Israel wapelekwa Uturuki
Wanaharakati kutoka Msafara wa Meli wa Global Sumud warejea Uturuki baada ya kuzuiliwa nchini Israel.

Wanaharakati waliokuwa kwenye msafara wa Flotilla kuelekea Gaza, ambao walizuiliwa kinyume cha sheria baada ya meli zao kushambuliwa katika maji ya kimataifa, wanapelekwa nchini Uturuki Alhamisi kwa ndege ya Shirika la Ndege la Uturuki.

Wanaharakati hao walihamishwa kutoka Gereza la Ketziot katika jangwa la Negev mpaka Uwanja wa Ndege wa Ramon, kusini mwa Israel, ambapo taratibu za kuwarudisha zilikamilika, chanzo cha Anadolu kimeeleza.

Wanaharakati hao baadae walipandishwa katika ndege tatu tofauti za Shirika la Ndege la Uturuki katika uwanja wa ndege wa Ramon.

Ndege ya kwanza iliyobeba wanaharakati hao iliondoka kuelekea jijini Istanbul kufuatia utaratibu ulioratibiwa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Uturuki, huku ndege nyengine zikitarajiwa kufika nchini Uturuki baadae Alhamisi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan amesema mapema Alhamisi kuwa ndege maalumu iliwekwa kwa ajili ya kuwarudisha raia wa Uturuki na washiriki wengine kutoka nchi ya tatu ambao walikuwa katika msafara wa Global Sumud Flotilla.

Msafara wa Flotilla wa misaada ya kimataifa umesema meli zote 50 zilizokuwa katika msafara zimeshikiliwa na Israel baada ya kushambuliwa katika maji ya kimataifa.

Msafara huo uliobeba watu 428 kutoka nchi 44, uliondoka Alhamisi iliyopita kutoka wilaya ya Uturuki ya Marmaris katika jaribio jipya la kuvunja kizuizi kilichowekwa na Israel dhidi ya Gaza tangu mwaka 2007.