Takriban watu sita wamejeruhiwa katika miji iliyo mstari wa mbele nchini Ukraine katika mashambulizi ya usiku yaliyo fanywa na Urusi.
"Mnamo Mei 1, Warusi walijeruhi wakazi wawili wa mkoa wa Donetsk: huko Kramatorsk na Siversk," Gavana wa Donetsk Pavlo Kyrylenko alisema kwenye Telegram.
Kyrylenko pia alisema maafisa wa Ukraine hawakuweza kuthibitisha idadi kamili ya waathiriwa katika miji ya Mariupol na Volnovas, kwa kuwa iko chini ya udhibiti wa Urusi.
Kando, Gavana wa Mykolaiv Vitaliy Kim alisema kwenye Telegram kwamba watu wawili walijeruhiwa katika kijiji cha Kutsurub kutokana na mashambulizi yaliyofanywa na Urusi.
"Baada ya kurusha makombora, hakuna umeme, gesi, maji, au mtandao kwenye makazi," Kim alisema, akibainisha pia kuwa moto uliripotiwa katika mji wa kusini wa Ochakiv lakini hakukuwa na majeruhi.
Wakati huo huo, utawala wa kijeshi katika eneo la kusini la Kherson ulisema kwenye Telegram kwamba makazi katika eneo hilo yalipigwa makombora mara 71 katika siku iliyopita, 11 kati ya hayo yaligonga katikati mwa mkoa.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa watu wawili walijeruhiwa.