Kamala Harris / Photo: AFP

Kamala Devi Harris alizaliwa 1964 na ni mwanasiasa na wakili ambaye amekuwa Makamu wa Rais wa 49 wa Marekani tangu 2021, akihudumu chini ya Rais Joe Biden.

Harris amekuwa mgombea wa chama cha Democratic katika Uchaguzi Mkuu wa Marekani wa 2024.

Amekuwa Makamu wa Rais wa kwanza mwanamke wa Marekani, na kumuweka katika historia ya kuwa miongoni mwa wanawake waliowahi kushika wadhifa wa juu kabisa katika historia ya nchi hiyo.

Baada ya kumaliza masomo yake mwaka 1990, Harris aliajiriwa kama naibu wakili wa wilaya katika Kaunti ya Alameda, California.

Na hapo ndio ilikuwa mwanzo wa safari yake katika utumishi wa umma.Mwaka 2002 Harris alichaguliwa kuwa mwanasheria wa wilaya ya San Francisco.

Na kuanzia 2011 alianza kazi kama Mwanasheria Mkuu wa California. Mwaka 2017 hadi 2021, aliwakilisha California katika Bunge la Seneti la Marekani.

Mwaka 2019, Harris alitafuta uteuzi wa mgombea urais chini cha Chama cha Demokrat kwa ajili ya uchaguzi wa mwaka 2020, lakini baadae alijiondoa katika kinyang'anyiro hicho kabla ya kura za mchujo.

Baadae Rais Biden alimuingiza katika kambi yake na kumchagua kama mgombea wake mwenza, na hatimae kumshinda aliyekuwa mpinzani wao wakati huo Donald Trump na makamu wake Mike Pence, katika uchaguzi wa 2020.

Kufuatia kuchaguliwa kwake kama Makamu wa Rais wa Marekani alianza wadhifa wake mpya 2021.Sera zake za ndani na nje ni zile zile za mtangulizi wake Joe Biden.

Kamala Harris ameingia katika orodha ya wanawake walioacha alama ya ushupavu na ukakamavu katika historia ya taifa hilo.

TRT Afrika