Rais Kais Saied amekataa mkopo wa IMF / Picha: Reuters

Tunisia imelitaka Shirika la Fedha Duniani (IMF) kupitia upya masharti yake ya mikopo wakati wa kutoa mikopo kwa mataifa yanayoendelea hasa yale ya Afrika.

Rais wa nchi hiyo, Kais Saied, anadai baadhi ya masharti yaliyowekwa na IMF ni ya kuadhibu na ya kudhalilisha mataifa yanayokopa.

Mara kadhaa, IMF imezitaka nchi za Afrika kuondoa programu za ruzuku na pia kupanga upya ofisi za serikali ili iweze kuwapa mikopo.

Rais Saied, anasema ruzuku huzuia raia dhidi ya gharama kubwa ya maisha, na kwamba wakopeshaji wa kimataifa hawapaswi kuelekeza mataifa huru juu ya namna ya kuendesha mambo yao ya ndani.

“Hawa (wananchi) si idadi tu, ni wanadamu ambao utu wao lazima uhifadhiwe. hali ya sasa lazima igeuzwe ikiwa wanataka haki,” Rais Saied alisema aliposhiriki katika mkutano wa kilele wa Paris kuhusu ufadhili wa kimataifa siku ya Alhamisi.

Tunisia inatafuta kifurushi cha kuokoa uchumi wake, cha thamani ya karibu dola bilioni 2 kutoka kwa IMF.

Licha ya mkopo huo kutolewa mnamo Oktoba 2022, taifa hilo la Afrika Kaskazini limekataa kupokea hadi IMF itakapoondoa masharti yake "magumu".

Suluhisho

Rais Saied alisema Alhamisi kwamba ameanzisha mazungumzo na IMF kutafuta makubaliano, alipokutana na Mkurugenzi Mkuu wa IMF, Kristalina Georgieva wakati wa mkutano wa mabadiliko ya tabianchi jijini Paris.

"Nilimthibitishia kwamba maagizo ya IMF yanaweza tu kukubalika kulingana na mtazamo wa nchi yetu, kwa sababu hatuwezi kukubali maagizo ambayo ni kama kuweka kiberiti kwenye vilipuzi," Rais Saied aliliambia shirika la habari la Tunisia, TAP.

Mkuu huyo wa nchi aliongeza kwamba kukubaliana na shinikizo la IMF kuondoa ruzuku na kuunda upya mashirika ya umma, kunaweza kusababisha machafuko ya wenyewe kwa wenyewe nchini humo. "Sitaki umwagaji damu kama matukio ya Januari 1984," alisema.

Saied, hata hivyo, alisema kuwa Tunisia inazingatia kubadilisha jinsi mpango wake wa ruzuku unasimamiwa, akifichua kwamba kuna uwezekano wa kutoza kodi watu ambao "hawastahili." Alisema kwa sasa, "hakuna data ya nchi zinazostahili afueni."

Mkurugenzi mkuu wa IMF, Georgieva alisema anafahamu wasiwasi uliotolewa na mataifa ya Afrika, na ameahidi kutoa fedha zaidi kwa mataifa yanayoendelea.

Amesema kuwa, IMF "kwa mara ya kwanza katika historia yetu" inatoa ufadhili wa muda mrefu - na kipindi cha ulipaji deni cha miaka 20 na kipindi cha neema cha miaka 10.

TRT Afrika