Jumuiya ya Ulaya EU imepanga kutoa dola milioni 135 (Euro milioni 127) kama msaada Kwa Tunisia ikiwa ni sehemu ya mpango wake kwa nchi hiyo unaolenga kuimarisha mapambano dhidi ya uhamiaji haramu kutoka Afrika kwenda Ulaya.
EU imesema siku ya Ijumaa kuwa dola milioni 64 zitawasilishwa kwenye msaada wa bajeti kwa Tunisia, huku kifurushi kingine kikitolewa siku zijazo kikiwa chenye thamani ya takriban dola milioni 71 kinacholenga kuimarisha uwezo wa Tunisia kupambana na wafanyabiashara wa watu na kupiga jeki udhibiti wa mpaka.
Mwezi Julai, Tunisia na EU walitia saini mkataba wa "ushirikiano wa kimkakati" wa kupambana na uhamiaji haramu ukishirikisha kubadilishana msaada wa kifedha kufuatia ongezeko kubwa la boti zinazoondoka taifa hilo la Afrika Kaskazini kuelekea Ulaya.
EU imesema kupitia taarifa yake kuwa kifurushi cha hivi karibuni cha kifedha kitasaidia kurekebisha meli za kushika doria, utafutaji na uokoaji, magari na vifaa vyengine kwa walinzi wa Pwani ya Tunisia na vikosi vya wanamaji.
Aidha, taarifa hiyo iliongeza kuwa kiasi hicho cha fedha kitasaidia katika ulinzi wa wanaotafuta hifadhi nchini Tunisia kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa na kurudishwa kwa wahamiaji katika nchi zao za asili,
"Utoaji wa vyombo vipya, kamera za joto na misaada mengine ya uendeshaji, pamoja na mafunzo muhimu, pia umetabiriwa," Tume hiyo ilifafanua.
Mfano wa makubaliano na nchi nyingine
Rais wa tume ya Ulaya Ursula Von Der Leyen alisema mwezi Julai kuwa mkataba wake na Tunisia unaweza kutumika kama mfano wa makubaliano na nchi nyingine, kama EU inajitahidi kuzuia mtiririko usioidhinishwa wa wimbi la wakimbizi katika Mediterranean.
Hata hivyo, baadhi ya wabunge wa EU, viongozi wa upinzani nchini Tunisia na wanaharakati wa haki za binadamu wamekosoa mpango huo, huku wakisema kuwa hautazuia uhamiaji bali utaimarisha serikali ya rais Kais Saied, ambaye wanamshutumu kwa utawala wa kiimla.
Said alichukua madaraka mnamo 2021, akifunga bunge kabla ya kupitisha katiba mpya ambayo inampa takriban nguvu na mamlaka yote kabisa.
Amejitetea kwa kusema kuwa vitendo vyake ni halali, na ni muhimu kuokoa Tunisia kutokana na machafuko na ufisadi uliokithiri.