Na
Massoumeh Torfeh
Jumapili hii, rais mteule wa Iran Masoud Pezeshkian anatarajiwa kuidhinishwa na Kiongozi Mkuu Ali Khamenei. Tarehe 30 Juali, ataapishwa rasmi na bunge la nchi hiyo.
Haishangazi kwamba Pezeshkian, daktari wa upasuaji wa moyo mwenye umri wa miaka 69, alishinda uchaguzi wa rais nchini Iran. Kinyume na wachanganuzi wengi, mafanikio yake hayaonyeshi kurudi kwa zama za wanamageuzi.
Badala yake, kuchaguliwa kwake ni mwanzo wa mkakati mpya wa kiongozi mkuu wa Iran, Ali Khamenei, ambayo kiini chake ni suluhu ya kuokoa uso wa Iran na kuitoa katika kutengwa kimataifa na kuongeza ushiriki zaidi wa ndani wa umma katika siasa.
Mabadiliko yako mbele
Pezeshkian alizuiwa kugombea katika kinyang'anyiro cha urais mwaka wa 2021 na Baraza la Walinzi, baraza linaloundwa na makasisi na wanasheria 12 ambao wana mamlaka kubwa nchini Iran.
Baraza hilo huchunguza sifa za kidini na kimapinduzi za wagombeaji na limewazuia wanamageuzi wengi maarufu na wenye msimamo wa wastani kugombea katika chaguzi za hivi majuzi.
Ukweli ya kwamba Pezeshkian aliidhinishwa na baraza wakati wa duru hii mpya ya uchaguzi ni dalili ya kwanza ya wazi ya mabadiliko yaliyoongozwa na Kiongozi Mkuu Khamenei.
Hatua hiyo kwa hakika ilikuwa ni sehemu ya mkakati wa pande tatu wa kuwarejesha wapiga kura kwenye sanduku la kura, kurudisha uhalali wa utawala ulioharibiwa vibaya hasa miongoni mwa vijana na walio wachache, na kubuni sura ya ya siasa ya wastani ili kusaidia kurudisha Iran kwenye "ushirikiano" na nchi za Magharibi na kumaliza vikwazo vizito vya kiuchumi na benki.
Kama sivyo hivyo, Kiongozi Mkuu Khamenei hangedai uungwaji mkono kamili wa bunge kwa rais mpya katika hotuba yake ya kwanza kabisa baada ya uchaguzi.
"Ninasisitiza kwamba ninataka ushirikiano kamili katika bunge na rais mteule," Khamenei alisema. "Ikiwa atafanikiwa kuboresha uchumi, sera ya kimataifa na sera ya kitamaduni, basi mafanikio yake ni mafanikio yetu sote."
Wachambuzi walitabiri idadi ndogo zaidi ya waliojitokeza katika uchaguzi huo na licha ya juhudi zote za kuwashawishi, asilimia 60 ya watu hawakushiriki katika duru ya kwanza. Lakini mbinu ya kutumia mgombea wa mageuzi ilizaa matunda na katika duru ya pili, asilimia 50 ya waliojitokeza ilitosha kuiita rasmi.
Ushiriki mdogo ulikuwa sababu kuu ya wasiwasi kwa Iran, ambayo inapata uhalali wake kutoka kwa uwezo wake wa kukusanya umati wa watu inapohitajika.
Kwa mantiki hiyo hiyo, Pezeshkian si mpenda mageuzi na ushirikiano wake wa karibu na waziri wa mambo ya nje wa zamani Jawad Zarif ambaye alionekana tena nje ya uwanja wa kisiasa, unaonyesha tu mwelekeo wa kisiasa wa Iran katika miaka michache ijayo.
Ni kweli kwamba Pezeshkian alikuwa katika mabaraza mawili ya wanamageuzi kati ya 1997 na 2005. Lakini katika miaka 20 iliyopita kama mbunge mwenye msimamo mkali, amehamia upande wa kulia. Uhusiano wake wa karibu na waziri wa zamani wa mambo ya nje Zarif, akimwita gwiji wake na kumbusu mikono yake hadharani, ni shahidi wa mabadiliko haya.
Zarif mwenye uzoefu mkubwa katika mazungumzo na nchi za Magharibi amechaguliwa kuongoza Kamati ya Sera ya Ndani na Nje, ambayo ina jukumu la kupendekeza mawaziri wanaofaa zaidi kwa nyadhifa hizo. Jukumu hili na mchakato wa kuidhinisha wajumbe wote wa baraza la mawaziri unaonekena kuwa kazi ngumu.
Mahusiano ya kimataifa
Katika makala ya mwezi huu yenye jina la "Ujumbe wangu kwa ulimwengu mpya," Pezeshkian alisema ana mpango wa kufuata sera ya kigeni "inayoendeshwa na fursa" na kuunda "usawa katika uhusiano na nchi zote."
Aliweka wazi kwamba washirika wa karibu wa Iran ni China na Urusi, lakini akasisitiza kwamba "ushirikiani wa kimataifa" ni sehemu ya sera anazoziendesha.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Anthony Blinken tayari anachukua fursa ya kubadilisha sauti ya kutatua suala la nyuklia "kupitia diplomasia." Matokeo ya uchaguzi wa Marekani mwezi Novemba yatakuwa ya kufualitiwa kwa kina. Hata hivyo Iran inaweza kufanya kazi na mgombea yeyote.
Bila shaka, rais wa zamani Donald Trump anaweza kuwa mgumu zaidi kukabiliana naye kama mtu ambaye alijiondoa kutumia maamuzi ya kipekee na kinyume cha sheria katika mapatano ya nyuklia (JCPOA) mwaka 2018 na kujigamba kuhusu mauaji ya Kamanda Mkuu wa Kikosi cha Quds wa Iran, Qassem Soleimani, mwaka 2020.
Kwa hali yoyote, msingi tayari umewekwa. Waziri wa mambo ya nje wa Iran hayati Hossein Amir-abdolahian tayari ameanzisha mazungumzo ya siri na Wamarekani, na kupitia upatanishi kutoka Oman na Qatar. Waziri Mkuu wa Japan Fumio Kishida katika mazungumzo na Pezeshkian pia amejitolea kuwa mpatanishi wa kufufua JCPOA.
Kwa upande wa Ulaya pia, Pezeshkian anaacha mlango wazi: "Ninatarajia kushiriki katika mazungumzo yenye kujenga na nchi za Ulaya ili kuweka uhusiano wetu kwenye njia sahihi." Ana uwezekano wa kupata suluhu kupitia nchi kama vile Ireland na Uhispania ambazo zimejitolea kutambua Palestina kama taifa huru.
Muungano wa nguvu?
Maandamano hayo yaliikumba Iran katika kipindi cha miaka miwili iliyopita ambapo msichana mdogo wa Kikurdi, Mahsa Amini, aliuawa akiwa chini ya ulinzi wa polisi. Ilileta jamii ya Wakurdi wengi wa Sunni kuelekeza makabiliano na serikali kuu na kiongozi mkuu.
Wakati huo huo, asili ya Pezeshkian ya Kituruki inaweza kusaidia katika mvutano unaozuka na Jamhuri ya Azabajani. Iran imeishutumu Azerbaijan kwa kuchochea hisia za kutaka kujitenga kwa wakazi wa jimbo la Azerbaijan nchini Iran.
Marehemu rais Ebrahim Raissi, aliyefariki katika ajali ya helikopta, alifariki alipokuwa akielekea eneo la mpakani kutia saini makubaliano ya urafiki na ushirikiano na rais wa Azerbaijan, Ilham Aliyev, ili kumaliza mvutano huo.
Kwa nini mbinu mpya?
Kuna sababu tatu kuu za mkakati mpya wa Ayatollah. Kwanza, kundi tawala lina wasiwasi zaidi kuhusu ukosefu wa ushiriki wa kisiasa na ushiriki mdogo katika uchaguzi. Wababe wanapata uhalali wao kutoka kwa mamlaka ya kukusanya umati.
"Unapaswa kufanya kila juhudi kuongeza idadi ya wapiga kura, iwe ni katika mazingira ya chuo kikuu, mahali pa kazi, mazingira ya familia, na maeneo mengine kama hayo," Khamenei alisema katika hotuba ya hivi majuzi.
Pili, athari za vikwazo zimekuwa zikiongezeka zikiathiri uwezo wa watu wa kununua, huku kiwango cha juu cha ubadilishaji sarafu kikisababisha maudhiko na hasira.
Hii ni kweli hasa miongoni mwa vijana Wairani wa kisasa na wasomi ambao wakati huo huo wamekuwa wakipinga utawala na kiongozi mkuu juu ya kanuni zake kali za mavazi. Ukandamizaji mkubwa dhidi ya waandamanji, hata hivyo haujawanyamazisha.
Tatu, katika muongo mmoja uliopita Iran imepoteza wasomi wengi wa ngazi za juu wa kisiasa, makasisi na kijeshi. Kwa kutaja wachache, kuuliwa kwa Soleimani na Marekani mnamo 2020 ilikuwa na athari kubwa zaidi.
Lakini hii ilifuatiwa na shambulio la mwanasayansi mkuu wa nyuklia wa Iran, Mohsen Fakhrizadeh, na hivi karibuni zaidi wakati wa vita huko Gaza, makamanda kadhaa wakuu wa IRGC waliuawa huko Syria na Jordan. Zaidi ya hayo, marehemu waziri wa mambo ya nje Amir-Abdolahian aliuawa katika ajali ya helikopta pamoja na Rais Ebrahim Raissi.
Viongozi hawa walikuwa wamepiga hatua katika kufufua uhusiano na mataifa ya Kiarabu, haswa na Saudi Arabia kupitia msaada wa kutoka China.
Kwa hivyo, chama tawala kimepata pigo nyingi mno sambamba na hujuma kadhaa kwenye mipaka ya kaskazini, kusini na mashariki ya Iran. Uongozi wa Pezeshkian ukiwa na sura ya mageuzi hutoa utaratibu unaohitajika wa kuokoa muonekano wa Iran ili kurekebisha inapokua hamna budi.
Mwandishi, Dk. Massoumeh Torfeh, ni mshirika wa utafiti katika shule ya London School of Economics na Shule ya Oriental and African Studie, anajihusisha na masuala ya Iran. Zamani alikuwa msemaji wa Umoja wa Mataifa na mwandishi wa habari wa BBC, na ameandika kitabu kuhusu uhusiano wa Iran na Uingereza.