Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) ilishutumu "mauaji ya halaiki" huko Gaza, na kuzitaka nchi wanachama wake 57 kuiwekea Israel vikwazo katika azimio lililopitishwa mwishoni mwa mkutano wake wa Gambia.
Shirika hilo lilitoa wito kwa wanachama wake kuweka "vikwazo kwa Israel, mamlaka inayoikalia kwa mabavu, na kusimamisha usafirishaji wa silaha na risasi zinazotumiwa na jeshi lake kutekeleza uhalifu wa mauaji ya kimbari huko Gaza".
Azimio la Jumapili, lililoonekana na shirika la habari la AFP, liliwataka wanachama "kutumia shinikizo la kidiplomasia, kisiasa na kisheria na kuchukua hatua zozote za kuzuia uhalifu wa uvamizi wa kikoloni wa Israel, na vita vya mauaji ya kimbari vinavyoendesha dhidi ya watu wa Palestina, ikiwa ni pamoja na kuweka vikwazo".
Pia ilitoa wito wa "kusitishwa kwa mapigano mara moja, kudumu na bila masharti".
OIC iliyoanzishwa mwaka 1969 baada ya kuchomwa moto Msikiti wa Al Aqsa katika Jerusalem Mashariki inayokaliwa kwa mabavu, inalenga kuongeza mshikamano wa Waislamu, kuunga mkono mapambano ya Wapalestina na kutetea maeneo matakatifu ya Waislamu.
Mnamo Novemba 2023, ilikutana na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu huko Riyadh kwa mkutano wa kilele wa pamoja, kulaani vitendo vya vikosi vya Israeli huko Gaza, lakini ilijiepusha kuweka hatua za kuadhibu za kiuchumi na kisiasa dhidi ya Israeli.
Lakini Desemba 2023, OIC ilikaribisha hatua iliyoletwa na Afrika Kusini dhidi ya Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) ambapo iliishutumu kwa mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina.
Mkutano wa 15 wa kilele wa OIC, ulioanza siku ya Jumamosi, ulilenga mji mkuu wa Misri Cairo, ambako mkutano kuhusu mapendekezo ya usitishaji vita, unaohusishwa na kuachiliwa kwa mateka huko Gaza, ulifanyika mwishoni mwa juma hili bila maendeleo yoyote madhubuti.
Ni viongozi wachache tu wa Afrika waliohudhuria mkutano wa OIC ana kwa ana, viongozi wengi wa nchi wanachama 57 wakituma wawakilishi.
Vita vya Israel dhidi ya Gaza vilianza kufuatia shambulio la Hamas la Oktoba 7 ambalo lilisababisha vifo vya zaidi ya watu 1,170, kulingana na hesabu ya AFP ya takwimu rasmi za Israeli.
Tangu Oktoba 7, mashambulizi ya kijeshi ya Israel yameua takriban watu 34,683 huko Gaza, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, kulingana na wizara ya afya ya eneo hilo.