Mshindi wa Kombe la dunia (na Ujerumani) na mchezaji wa zamani wa Arsenal, Mesut Ozil amekuwa mmoja wa nyota waliozungumzia hali hiyo huku wanasoka maarufu wakitumia mitandao yao ya kijamii kuiunga mkono Palestina.
Wachezaji mbalimbali wametumia mitandao ya Facebook, Instagram na X, kuonyesha mshikamano wao na Palestina.
"Naombea ubinadamu. Naombea amani. Watu wasio na hatia na hasa watoto wasio na hatia wanapoteza maisha yao katika vita-pande zote mbili. Inavunja moyo na kuhuzunisha. TAFADHALI ACHA VITA!!!". Aliandika kwneye mtandano wa X.
Mesut Ozil amekuwa akizungumzia suala la Palestina mara kwa mara.
Wachezaji wa Algeria akiwemo Riyad Mahrez, Saïd Benrahma na Ahmed Touba walishikilia bendera ya Palestina baada ya mechi yao dhidi ya Cape Verde. Mabingwa hao wa Afcon 2019, waliishinda Cape Verde 5-1 katika mechi ya kirafiki iliyochezwa alhamisi Oktoba 12, Constantine.
Huku hayo yakijiri, mchezaji wa Algeria Youcef Atal ametishiwa na meya wa Jiji la Nice Christian Estrosi aliyetumia mtandao wa X, kulaani maandiko ya mwanasoka huyo yalionekana kuunga mkono Palestina.
"Natarajia Youcef Atal, kuomba msamaha na kulaani magaidi wa Hamas kwa kukubali kutumiwa vibaya. Ikiwa hatofanya hivyo, hawezi kuwa tena na nafasi ya kuiwakilisha timu yetu ya Nice". Aliandika
Mbali na hayo, mabingwa wa Ligi ya Mabingwa wa soka barani Afrika, kutoka Misri Al-Ahly, ambayo iliinua taji lake la 11 la Afrika kwa ushindi wa 3-2 dhidi ya Wydad Casablanca ya Morocco, imetoa taarifa kwenye ukurasa wake wa X, ikiandika kuwa pamoja na Palestina.
Mashabiki wa klabu ya soka ya Morocco Raja CA walishangilia na kuunga mkono Palestina huku wakiinua bendera za Palestina wakati wa mechi ya klabu hiyo iliyopigwa jumapili iliyopita kwenye Uwanja wa soka wa Mohammed V mjini Casablanca.
Mashabiki wa timu ya taifa ya soka ya Bolivia nao walitoa bendera ya Palestina kwenye mechi kati ya Ecuador na Bolivia.
Wakati huo huo, mashabiki wa Celtic wameunga mkono kwa kushikilia bendera za Palestina wakati wa mechi ya ligi ya Scotland kati ya Celtic na Kilmarnock huko Celtic Park, mnamo Oktoba 07, 2023, mjini Glasgow, Scotland.
Nchini Qatar, wachezaji kutoka timu za Al Gharafa na Al Duhail, wakiwemo mchezaji wa zamani wa Kimataifa wa Algeria Yacine Brahimi, walishikilia bango la kuunga Mkono Palestina kabla ya mechi yao ya Kombe La Qatar likiwa limeandikwa, "Palestina, daima na milele katika mioyo yetu".
Wakati huo huo, rais wa shirikisho la soka duniani FIFA, Gianni Infantino ametoa salamu za rambirambi kwa mashirikisho ya soka ya Israel na Palestina.
"Ulimwengu wa soka unasimama imara katika mshikamano na watu wa Israeli na Palestina, na kwa wahasiriwa wote wasio na hatia ambao wameathirika na isiyoelezeka."
Kufikia mapema Jumapili Idadi ya watu waliouawa katika mashambulizi ya Israel kwenye Ukanda wa Gaza tangu Oktoba 7 imeongezeka hadi 2,329.