Shirika la Red Crescent la Palestina lilisema lori 30 za ziada za misaada ziliingia Gaza kupitia kivuko cha mpaka cha Rafah na Misri.
"Timu zetu zimepokea leo lori 30 za msaada wa kibinadamu kupitia kivuko cha Rafah," ilisema katika taarifa yake Jumamosi.
Ilisema malori matatu kati ya hayo ni ya Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu, 19 ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Palestina (UNRWA) na nane iliyobaki ya Jumuiya ya Red Crescent iliyotumwa kutoka Misri.
Taarifa hiyo ilibainisha kuwa malori manne yamebeba dawa na vifaa vya tiba, huku mengine yakiwa na vyakula, maji na misaada.
Ilibainisha kuwa idadi ya malori yaliyoingia Gaza tangu Oktoba 21 ilifikia 451. Jeshi la Israel bado linazuia kuingia kwa mafuta Gaza.
Idadi ya vifo inaongezeka
Chini ya mzingiro wa miaka 16 wa Israel dhidi ya Gaza, lori 500 za mizigo, ikiwa ni pamoja na lori 45 za mafuta zilitumika kuingia Gaza kila siku.
Lakini hayo yote yalisimama tangu kuzuka kwa mapigano Oktoba 7, ukiiondoa Gaza yenye uhaba mkubwa wa bidhaa za kimsingi, ikiwa ni pamoja na mafuta yanayohitajika sana kwa hospitali.
Jeshi la Israel limepanua mashambulizi yake ya angani na ardhini kwenye Ukanda wa Gaza, ambao umekuwa chini ya mashambulizi ya angani tangu mashambulizi ya kushtukiza ya kundi la muqawama la Palestina, Hamas, tarehe 7 Oktoba.
"Idadi ya waliouawa kutokana na uvamizi wa Israel kwenye Ukanda wa Gaza tangu Oktoba 7 ni 9,500, ikiwa ni pamoja na watoto 3,900 na wanawake 2,509," Salama Marouf, mkuu wa Ofisi ya Vyombo vya Habari Gaza, alisema katika mkutano na waandishi wa habari. Takriban Waisrael 1,540 wameuawa.