Kiongozi wa Hamas Ismail Haniyeh ameuawa nchini Iran asubuhi ya leo, kundi la Palestina Hamas limethibitisha. / Picha: Reuters

Ismail Haniyeh, mkuu wa kundi la muqawama la Palestina Hamas, na mmoja wa walinzi wake waliuawa katika makazi yao Tehran mapema Jumatano, kwa mujibu wa Walinzi wa Mapinduzi ya Iran.

Hamas na maafisa wa Iran wamethibitisha kuwa Haniyeh aliuawa wakati wa uvamizi wa Israel uliolenga nyumba yake katika mji mkuu wa Iran.

Mauaji hayo yanaashiria ongezeko kubwa la mzozo wa kikanda huku wasiwasi juu ya uwezekano wa hatua za kulipiza kisasi ukiongezeka.

Haya hapa ni baadhi ya maoni kutoka duniani kote kuhusu mauaji hayo.

Palestina

Rais wa Palestina Mahmoud Abbas amelaani mauaji ya kiongozi wa Hamas Ismail Haniyeh, kwa mujibu wa runinga ya taifa ya WAFA.

Abbas alilaani mauaji ya Haniyeh kama "kitendo cha woga na maendeleo ya hatari."

Afisa mkuu wa Palestina Hussein al Sheikh katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan pia alilaani mauaji ya Haniyeh kama "kitendo cha woga."

"Tunashutumu vikali na kulaani mauaji ya mkuu wa Ofisi ya Kisiasa, kiongozi wa kitaifa, Ismail Haniyeh," mkuu wa masuala ya kiraia wa Mamlaka ya Palestina aliandika kwenye X.

"Tunakichukulia kama kitendo cha woga, hii inatusukuma kuendelea kuwa na msimamo thabiti mbele ya uvamizi huo, na ulazima wa kufikia umoja wa vikosi na mirengo ya Palestina."

Uturuki

Uturuki siku ya Jumatano alilaani "mauaji ya aibu" ya kiongozi wa kisiasa wa Hamas Ismail Haniyeh - mshirika wa Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan - wizara ya mambo ya nje ilisema katika taarifa.

"Tunalaani mauaji ya kiongozi wa ofisi ya kisiasa ya Hamas, Ismail Haniyeh, katika mauaji ya aibu huko Tehran," wizara hiyo ilisema, na kuongeza kuwa "shambulio hili pia linalenga kueneza vita vya Gaza katika mwelekeo wa kikanda".

Urusi

Naibu mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi alilaani mauaji ya Ismail Haniyeh kama "mauaji yasiyokubalika ya kisiasa" ambayo huenda yakazidisha mvutano wa kikanda.

"Haya yote ni mabaya sana. Haya ni mauaji ya kisiasa yasiyokubalika kabisa, na yatasababisha kuongezeka zaidi kwa mivutano," Bogdanov aliambia shirika la habari la serikali ya Urusi, RIA Novosti.

Kilichotokea kitakuwa na athari mbaya katika mazungumzo ya Doha, Bogdanov alionya.

Marekani

Chombo cha habari chenye makao yake nchini Marekani CNN kilisema Ikulu ya Marekani inafahamu kuhusu taarifa za kuuawa kwa mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Hamas Ismail Haniyeh.

"Ikulu ya White House imeona ripoti za kiongozi wa kisiasa wa Hamas Ismail Haniyeh kuuawa nchini Iran, msemaji alisema lakini alikataa kutoa maoni zaidi mara moja," CNN iliripoti.

TRT World