Rais mteule Masoud Pezeshkian akitoa hotuba baada ya kula kiapo chake katika hafla iliyofanyika bungeni mjini Tehran, Iran, Jumanne, 30, 07,2024. /Picha: AP

Na

Ata Şahit

Mnamo tarehe 11 Agosti, Rais mteule wa Iran Masoud Pezeshkian aliwasilisha baraza lake la mawaziri lililopendekezwa kwa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu - Bunge la Iran - kwa kupigiwa kura ya imani.

Kwa mujibu wa sheria za Iran, Spika wa Bunge atasoma barua ya utangulizi ya rais, na baada ya hapo hati zinazoambatana nazo zitatumwa kwa kamati maalumu zinazofaa kwa ajili ya ukaguzi.

Kamati hizi zina jukumu la kutathmini sifa, historia, na programu zinazopendekezwa za kila mgombea uwaziri na kisha kuwasilisha matokeo yao katika ripoti kwa Spika. Ripoti hii pia itachapishwa na kusambazwa kwa wabunge wote kwa ajili ya mapitio yao.

Wiki moja baada ya kuanzishwa kwa serikali, mfululizo wa vikao vya bunge vitajadili sera na programu za jumla za serikali na kupiga kura ya imani katika baraza la mawaziri lililopendekezwa.

Katika kipindi hiki, mawaziri walioteuliwa pia watawasilisha programu zao kwa kamati zinazohusika na kujibu maswali yoyote kutoka kwa wanakamati.

Mchakato huo utafikia kilele baada ya kila waziri kupiga kura ya imani, ikifuatiwa na kura ya pamoja ya imani kwa baraza zima la mawaziri.

Baraza la mawaziri lililopendekezwa na Pezeshkian

Baraza la Mawaziri lililopendekezwa limezua mjadala mkali katika vyombo vya habari vya Irani, ukiwa umejikita zaidi katika swali la iwapo asili ya kisiasa ya waliopendekezwa inalingana na ahadi za Pezeshkian alizotoa wakati wa kampeni yake ya uchaguzi.

Hasa, umri wa wastani wa wajumbe wa baraza la mawaziri waliopendekezwa ni karibu miaka 60. Kuna mwanamke mmoja tu aliyeteuliwa, na baraza la mawaziri la nchi yenye Washia wengi halina uwakilishi wowote wa Sunni.

Zaidi ya hayo, watu watatu wakuu kutoka katika baraza la mawaziri la Rais wa zamani Ebrahim Raisi wameteuliwa tena kuwa mawaziri. Hii imesababisha madai kwamba baraza la mawaziri la Pezeshkian linapingana na ahadi zake za kampeni za kufufua upya, usawa wa kijinsia, uwazi wa kisiasa na mabadiliko.

Pamoja na mazungumzo yake yote makubwa kuhusu mabadiliko, baraza la mawaziri linalopendekezwa linaonekana kuwa na sifa za serikali yenye msimamo wa wastani, inayoegemea kwenye uhafidhina badala ya ile iliyoahidiwa ya mageuzi.

Hii imesababisha ukosoaji kutoka kwa wapenda mageuzi wa nchi, na Jumuiya ya Mageuzi ya Irani ilitoa barua muhimu ya wazi kwa Pezeshkian.

"Katika mchakato wa kuunda serikali mpya, hakikisha kwamba taratibu potofu hazisababishi kutengwa kwa watu wenye talanta na kusababisha umma kukosa imani na uamuzi wao wa kukuchagua," ilisema barua hiyo.

Azar Mansoori, mkuu wa Jumuiya ya Mageuzi, pia alielezea wasiwasi wake binafsi kupitia mtandao wa X, akisema, "Baraza la mawaziri hili linapaswa kuwa ishara ya mabadiliko, na sio kuendeleza hali iliyopo."

Upinzani dhidi ya uteuzi wa Pezeshkian ulienea zaidi ya hata ule wa Mrengo wa Mageuzi, huku waziri wa zamani wa mambo ya nje Mohammad Javad Zarif, ambaye Pezeshkian alimteua kama Makamu wa Rais wa Mikakati, pia alitangaza kujiuzulu kwake.

Ingawa maendeleo ya haraka yanaonyesha changamoto zinazoongezeka kwa uongozi wa Pezeshkian juu ya baraza lake la mawaziri lililopendekezwa, misimamo ya wastani na ya kihafidhina ya serikali yake haishangazi.

Hakika, katika mahojiano ya hivi majuzi, Pezeshkian alionyesha kuwa baraza la mawaziri litakuwa na watu walioidhinishwa na Kiongozi Mkuu.

Uchambuzi wa hali ya kisiasa ya ndani ya Iran unaonyesha kuwa, changamoto kuu zinazoikabili serikali ya Pezeshkian ni pamoja na kuongezeka kwa mpasuko kati ya dola na jamii, masuala ya uhalali, migogoro ya maji na mazingira, uhaba wa nishati na wasiwasi wa uhamiaji.

Miongoni mwa haya, suala la uhalali wa kisheria ya serikali linaweza kubishaniwa kuwa ndilo linalosisitiza zaidi.

Uchunguzi wa karibu wa uhusiano kati ya serikali na jamii nchini Iran unaonyesha kuwa umedorora kwa kiwango cha juu kabisa katika historia ya jamhuri.

Hili linadhihirika zaidi katika kupungua kwa idadi kubwa ya wapiga kura.

Changamoto za sera za kigeni

Miongoni mwa changamoto za kimsingi ambazo Iran inapaswa kushughulikia katika sera za kigeni ni kutengwa kwake katika jukwaa la kimataifa.

Wakati wa majadiliano kwenye televisheni ya taifa ya Irani, Pezeshkian alisema mengi.

“Kanuni inayoongoza ya sera yetu ya mambo ya nje itakuwa ni maslahi ya watu wa Iran. Lengo la sera yetu ya mambo ya nje haitakuwa ni kuishi tu; tunalenga kuhama kutoka maisha ya kiwango cha chini hadi maisha ya kiwango cha kuridhisha, kutoa fursa za ukuaji kwa watu wetu. Hatutaki kubaki pekee duniani.”

Kimsingi, Pezeshkian ameahidi kufuata sera ya kigeni inayoendana na kanuni za kimataifa.

Kutengwa kwa Iran na jumuiya ya kimataifa kunawakilisha suala la msingi linaloathiri moja kwa moja siasa za ndani za nchi. Tatizo hili kimsingi linatokana na vikwazo vilivyowekwa na Marekani.

Kwa hivyo, Iran haitaweza kupata maendeleo makubwa ikiwa suala la vikwazo hivi vya Amerika halitatuliwa.

Uchambuzi wa sera za kigeni za Iran katika miongo miwili iliyopita unadhihirisha kuwa suala la vikwazo limetiliwa umuhimu mkubwa zaidi.

Sababu kuu ya vikwazo hivi ni wasiwasi wa kimataifa kuhusu mpango wa nyuklia wa siri wa Iran.

Wasomi wengi wa Iran wanahoji kuwa kushindwa kulishughulikia suala hili na vikwazo vinavyoendelea vinawakilisha kikwazo kikubwa zaidi kwa maendeleo ya nchi.

Wanadai kuwa hali hii sio hatari ya kiuchumi pekee, na pia inaathiri kwa kiasi kikubwa hali ya kisiasa ya ndani ya Iran na mienendo ya usalama ya kikanda.

Sayyed Abbas Araghchi, aliyekuwa akihusika kwenye majadiliano ya nyukilia alipendekezwa na Pezeshkian kuwa waziri wa mambo ya nje, anajulikana kwa kujitolea kwake kufanya mazungumzo na jumuiya ya kimataifa na uungaji mkono wake mkubwa kwa makubaliano ya nyuklia ya 2015, ambayo yalitupiliwa mbali na rais wa zamani Donald Trump.

Kwa mtazamo wa Araghchi, kutozingatia kwa Iran mikataba na kanuni za fedha za kimataifa kunatatiza uwepo wake katika jukwaa la kiuchumi wa dunia katika zama za mifumo iliyounganishwa wa kimataifa ambapo kanuni za kimataifa huathiri kwa kiasi kikubwa shughuli na sera za kitaifa.

Kwa hivyo, Iran inapaswa kushughulikia suala hili kwa njia ya mazungumzo.

Araghchi ni mmoja wa watu wachache wenye uwezo wa kuanzisha na kuhitimisha kwa mafanikio mazungumzo kama haya. Anakubalika sana na watu wa wa mrengo wa wastani na pia amepata kibali cha Kiongozi Mkuu.

Hakika, uteuzi wa Araghchi kama waziri wa mambo ya nje unaashiria mwelekeo wa Iran kuelekea sera ya nje ya wastani zaidi.

Je, Araghchi anaweza kufanikiwa pale ambapo wengine wameshindwa?

Hilo ndilo gumu zaidi wakati Iran inatazamia kujenga mustakabali wake chini ya kiongozi mpya

Mwandishi Ata Şahit ni mwanahabari mkuu wa TRT.

TRT World