Ripoti ya mwisho ya tume inayochunguza ajali ya helikopta iliyosababisha kifo cha aliyekuwa Rais wa Iran Ebrahim Raisi mwezi Mei imehitimisha kuwa tukio hilo lilisababishwa na hali mbaya ya hewa.
Tume hiyo, iliyojumuisha wataalam maalumu wa kijeshi na raia, iliwasilisha ripoti hiyo Jumapili, ikihusisha ajali hiyo na "hali tata ya hali ya hewa na anga" ya kawaida ya majira ya kuchipua kaskazini magharibi mwa Iran.
Raisi, pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa wakati huo Hossein Amirabdollahian na wenzi wao, wote waliangamia wakati helikopta waliyokuwa wakisafiria ilipoanguka katika milima karibu na mji wa Tabriz mnamo Mei 19.
Kundi hilo lilikuwa likirejea kutoka kwa sherehe kwenye mpaka wa Azerbaijan kufuatia uzinduzi wa mradi mkubwa wa bwawa.
Kufuatia ajali hiyo, tume iliundwa kuchunguza sababu na maelezo ya ajali hiyo, ambayo baadaye ilisababisha uchaguzi wa rais kufanyika nchini humo.
'Maelekezo yalifuatwa'
Ripoti ya tume hiyo ilisema kuwa hali mbaya ya hewa kaskazini mwa Iran wakati wa majira ya masika ilisababisha kutokea kwa ukungu mwingi na kusababisha helikopta hiyo kugongana na mlima.
Ripoti ilionyesha kuwa nyaraka na kumbukumbu zote zinazohusiana na matengenezo ya helikopta zilipitiwa, na kila kitu kilipatikana kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa.
Zaidi ya hayo, nyaraka na mawasiliano yanayohusiana na misheni ya timu ya ngazi ya juu ndani ya helikopta yalionekana kuwa "kwa kufuata maagizo, miongozo, sheria na viwango muhimu."
Ripoti hiyo ilithibitisha kuwa helikopta hiyo "ilifuata njia iliyopangwa na haikukengeuka," ikisema kwamba ripoti za hali ya hewa kutoka siku ya ajali na siku iliyotangulia pia zilichunguzwa.
Taarifa kutoka kwa kinasa sauti cha chumba cha marubani (CVR) na kinasa sauti cha ndege (FDR) zilichanganuliwa, na ikathibitishwa kuwa hakuna ujumbe wa dharura au ishara za dhiki zilizotolewa na rubani.
Uchunguzi huo haukupata ushahidi wowote wa shughuli zinazotiliwa shaka au dalili za hujuma, ikiwa ni pamoja na uwezekano wa helikopta hiyo kulengwa au kukabiliwa na vita vya kielektroniki.
Raisi alihudumu kama rais wa Iran kwa miaka mitatu na akarithiwa na Masoud Pezeshkian kufuatia ushindi wake katika uchaguzi wa rais uliofanyika mwezi Juni.