Donald Trump akila kiapo mbele ya Jaji Mkuu John Roberts./Picha: Wengine

Sasa ni rasmi.

Donald Trump ameapishwa rasmi kama Rais wa 47 wa Marekani katika hafla iliyofanyika Januari 20 ndani ya jengo la bunge la nchi hiyo.

Rais Trump alikula kiapo mbele ya Jaji Mkuu John Roberts, huku akiwa amegusa Biblia mbili zilikuwa zimeshikwa na mke wake, Melania Trump.

Moja ya Biblia hizo iliwahi kutumika na Rais wa zamani wa nchi hiyo Abraham Lincoln wakati wa uapisho wake mwaka 1861 na Barack Obama mwaka 2009 na 2013.

Hapo awali, Trump na kiongozi aliyemaliza muda wake Joe Biden waliongozana pamoja kwenye hadi kwenye ukumbi wa Bunge la nchi huku hafla hiyo ya uapisho ikifanyika kwenye ukumbi wa ndani kutokana na hali mbaya ya hewa.

Mapema Januari 20, wake za wawili hao walikutana kwa kikombe cha chai ndani ya Ikulu ya nchi hiyo.

"Karibu nyumbani,” Biden alimwambia Trump huku mke wake Jill Biden akisalimiana na wapangaji hao wapya wa Ikulu ya Marekani.

'Kuvunja miiko'

Licha ya Marekani kuwa na utamaduni wa kutokualika viongozi wa nchi zingine wakati wa hafla ya uapisho, hali ilikuwa tofauti kidogo siku ya Januari 20 kwani Rais wa Argentina Javier Milei na Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni, walipata bahati ya kuhudhuria.

Hata hivyo, kama ilivyokuwa mwaka 1985 wakati wa Rais Ronald Reagan, uapisho wa Trump ulifanyika sehemu ya ndani ya majengo ya bunge kutokana na hali mbaya ya hewa.

TRT Afrika