Baadhi ya wanariadha mahiri wamelaumiwa kwa kutojua maana ya majina yao au kutojisumbua kutafuta jinsi ya kutamka./ Picha: Reuters 

Na Dayo Yussuf

Kupanda jukwaa kwenye hafla kubwa ni kitu kinabakia milele katika kumbukumbu yako.

Michezo haswa huashiria mafanikio makubwa kwa sababu hii inamaanisha kuwa unashinda makumi, au wakati mwingine mamia ya washiriki wengine kwenye uwanja wako. Ina maana kuwa wewe sasa unatajika miongoni mwa magwiji.

Lakini nini kinatokea wanapokosea jina lako. Hili anafahamu fika Ferdinand Omanyala na Wakenya wenzake pale mtangazaji wa shughuli katika hafla ya ufunguzi ya Olimpiki ya Paris 2024, alipo pondaponda jina la Omanyala na kulitaja ndivyo sivyo.

Jeshi la mitandao ya kijamii la Kenya (Kenyans On Twitter, KOT) lilifanya vurugu mtandaoni likielezea kuchukizwa kwao na kile walichokiita ukosefu wa heshima, kiburi, na hata wengine walienda mbali zaidi kuiita wivu.

Sawa, pengine jina la Omanyala linaonekanya la kuwakanganya wengi wasio na uzoefu. Lakini hiki sichoo kisa cha pekee.

 Iwapo jina sio la asili la Magharibi, una uhakika Wazungu wataliponda matamshi yake./ Picha : X-  Shola Shoretire

‘’Kuna Mwanasoka wa Nigeria anayechezea Manchester United. Jina lake ni Shoretire. (Linatamkwa: SHOW- REH – TEEREH). Lakini kila mara wanamwita SHOW-TAYA, na hakuna aliyejaribu kusahihisha’’ asema Mohammed Mowiz Suleiman, Mtangazaji na mchambuzi wa Michezo kwa muda mrefu nchini Nigeria. ‘’Imekuwa ikitokea kwa muda mrefu. Na itaendelea isipokuwa jambo lifanywe kwa makusudi kuhusu hilo,’’ anaiambia TRT Afrika.

Mifano ni mingi. Kiufupi unaweza kusema kwa asili mia kubwa, iwapo jina sio la asili la Magharibi, una uhakika Wazungu wataliponda matamshi yake.

Jina la mtu ni utambulisho wake na linakuja na hisia fulani ya fahari na turathi. Kejeli yoyote ya jina la mtu, iwe kwa kukusudia au vinginevyo, inaweza kueleweka vibaya kama kukosa heshima.

‘’Kwa watu wengi wa nchi za Magharibi, nadhani ni suala la kujiona bora, au kutojali,’’ anasema Mowiz. ‘’Lakini ni jukumu lako wewe Mwafrika, unavyopendelea kutamkwa jina lako, ukiwauliza, watatamka sawa.’’ Anasema.

Ingawa makosa haya ya jina ni ya kawaida, inakera zaidi unapoisikia kutoka kwa Mwafrika mwenyewe. Baadhi ya wanariadha mahiri wamelaumiwa kwa kutojua maana ya majina yao au kutojisumbua kutafuta jinsi ya kutamka.

‘’Tunaye mwanasoka huyu wa Kimataifa wa Nigeria ambaye hakuweza hata kutamka jina lake kwa usahihi. Jina lake ni Olaoluwa "Ola" Aina, (Tamka: Ola –Oloua- Ay-no) lakini anajiita Ola Aynah.) Kawaida wazo mamengi huingia katika kumtaja mtoto, wakati mwingi ni hisia zenye maana zaidi.

Watu wengine wamepewa majina ya watu maalum sana katika maisha yetu, au ambao tumewahi kupishana nao hapo awali na kuacha athari.

Wengine wanaweza kuitwa kwa jina la jamaa maalum awe amefariki au bado yupo hai. Au kwa wengine, wanawapa watoto wao majina kwa nia kuwa jina hilo litawapa hamasisho katika maisha majina yao.

‘’Majina haya yote huwa na maana na hivyo ni juu ya mwanariadha kuhakikisha jina lake linatamkwa sawa. Kwa mfano mtoto wa Kiarabu hata analelewa wapi au mtoto wa Kituruki analelewa wapi, watakueleza wazi jinsi ya kutamka jina lake, lakini kwa Mwafrika wa kawaida hata utamke jina lake anaona ni poa tu, anaridhika,'' analalamika Mowiz.

Vyombo vikubwa kama vile ligi kuu ya Uingereza vitawauliza wachezaji kutaja majina yao ili watu waweze kulirekebisha.

Ni jambo la kuchekesha kuona tukio kubwa kama Olimpiki halichukulii suala hili kwa umuhimu.

Wakati mwingine waendeshaji shughuli na watangazaji wenyewe watafanya juu chini kuuliza jinsi majina wasio na uzoefu nayo yanatamkwa.

‘’Naona aibu sana binafsi ninapokosa kutamka jina la mwanariadha fulani kwa usahihi. Ninajitolea kuona jinsi inavyotamkwa katika nchi yake, nauliza maswali,’’ anasema Mowiz.

Kufanya kazi kama mtangazaji wa michezo, jambo moja unalohakikishiwa ni kukutana na majina ambayo hujawahi kuyasikia. Ikiwa haujajiandaa, utakutana na jina katikati ya sentensi ukiwa hewani. Na huo ndio wakati mbaya zaidi. Jina linachinjwachinjwa bila huruma.

Kama mtangazajiw a michezoi, Ikiwa haujajiandaa, utakutana na jina katikati ya sentensi ukiwa hewani. / Picha : Reuters 

Majina kama vile Santi Carzola, mchezaji wa zamani wa Arsenal, au Emmanuel Adebayor, au mchezaji wa zamani wa kulipwa wa Nigeria Nwankwo Kanu.

Kwa hivyo unaweza kuelewa hasira waliyo nayo Wakenya wakati, kwenye Michezo ya Olimpiki ambapo wanang'ara kwa kushinda medali nyingi zaidi na kuvunja rekodi, wanasikia majina ya wanariadha wao kama Kipng’eno, Kipyegon, Keter, Cherotich, au Omanyala yakichinjwa.

‘’Nadhani wanariadha wengi hawajali. Wanazingatia mchezo na mashindano yao na ni vigumu kusikiliza matangazo. Kwa hivyo huenda wasiathirike katika mashindano kwa jinsi jina lao lilivyoitwa,’’ anasema Mowiz.

Jukumu huwa kwa watangazaji ikiwa wanataka kuonekana kuwa wajanja au wakati mwingine inawapa ile taswira kuwa wanafahamiana na wanariadha ikiwa wanaweza kutamka majina vizuri.

Lakini baada ya yote , Mowiz anasema inahitaji kutoka kwa wanariadha wenyewe kabla ya sisi wengine kulalamika kwa niaba yao.

‘’Wakati fulani kwao ni jambo la dhihaka, hata wanapozungumza watafanya mzaha kuhusu jinsi Wazungu wanavyoita majina yao, au jinsi Waarabu wanavyowaita,’’ Mowiz anaiambia TRT Afrika.

TRT Afrika