Waasi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wameimarisha udhibiti wa eneo la Rubaya la uchimbaji madini ya coltan, na kuweka ushuru wa uzalishaji unaokadiriwa kupata karibu dola 300,000 katika mapato ya kila mwezi, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilisikia Jumatatu.
Vuguvugu la M23, shirika linaloongozwa na Watutsi linalodaiwa kuungwa mkono na Rwanda, liliteka eneo hilo, ambalo linazalisha madini yanayotumika katika simu za kisasa na kompyuta, kufuatia mapigano makali mwezi Aprili.
Bintou Keita, mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DR Congo, aliliambia Baraza la Usalama kuwa biashara ya madini katika eneo la Rubaya inachangia zaidi ya 15% ya usambazaji wa tantalum duniani.
DR Congo ndiyo nchi inayoongoza duniani kwa kutengeneza tantalum ambayo inachukuliwa kuwa muhimu sana na Marekani na Umoja wa Ulaya.
'Inahitaji kusitishwa '
"Hii inazalisha wastani wa dola 300,000 katika mapato kwa mwezi kwa kundi lenye silaha," Keita alisema. "Hili linahusu sana na linahitaji kukomeshwa."
"Uharibifu wa uhalifu wa maliasili za DRC zinazotoroshwa nje ya nchi unaimarisha makundi yenye silaha, kuendeleza unyonyaji wa raia, baadhi yao wakigeuzwa watumwa, na kudhoofisha juhudi za kuleta amani," Keita aliongeza.
Rasilimali nyingi za madini za DR Congo ziko mashariki, eneo ambalo limekumbwa na migogoro ya ardhi na rasilimali kati ya makundi kadhaa yenye silaha. Hali imekuwa mbaya tangu kuanza tena kwa uasi wa M23 mnamo Machi 2022.
Maelfu wameuawa na zaidi ya milioni moja wamekimbia makazi yao tangu kuzuka upya kwa mapigano.
'Wajasiriamali wa kijeshi'
Watengenezaji wanachunguzwa ili kuhakikisha kuwa metali zinazotumika katika bidhaa kama vile kompyuta za mkononi na betri za magari yanayotumia umeme hazitolewi kutoka maeneo yenye migogoro kama mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Keita alisema kuwa faida kutokana na uchimbaji madini inaongezeka, vikundi vilivyojihami vimekuwa wajasiriamali wa kijeshi, na kuwafanya kuwa na nguvu zaidi kijeshi na kifedha.
"Isipokuwa vikwazo vya kimataifa vimewekwa kwa wale wanaonufaika na biashara hii ya uhalifu, amani itasalia kutoweka, na raia wataendelea kuteseka," Keita alisema.