Madagascar imemkamata mwanajeshi wa zamani wa Ufaransa anayeshtumiwa kwa kusababisha ukosefu wa usalama katika nchi hiyo, ikiwemo kuchochea maafisa wa usalama kufanya uasi na kuharibu miundombinu kwa lengo la kusababisha kukosekana kwa umeme, mamlaka zimesema.
Kwingineko, wizara ya mambo ya nje ya Madagascar imesema siku ya Jumanne kuwa imemtaka afisa mmoja wa ujasusi katika ubalozi wa Ufaransa mjini Antananarivo kuondoka nchini humo kwa mienendo yanayoonekana kuwa kinyume na hadhi yake ya mwanadiplomasia.
Rais wa Madagascar Michael Randrianirina aliingia madarakani mwezi Oktoba mwaka jana, baada ya maandamano ya vijana dhidi ya mtangulizi wake, Andry Rajoelina.
Ubalozi wa Ufaransa haujatoa taarifa kuhusu tukio hilo.
Amezuiliwa kabla kushtakiwa
Naibu Mwendesha mashtaka Nomenarinera Mihamintsoa Ramanantsoa ametoa taarifa kwa njia ya video iliotolewa siku ya Jumanne kuwa mwanajeshi huyo wa zamani wa Ufaransa, Guy Baret, amezuiliwa kabla ya kushtakiwa katika gereza lenye ulinzi mkali la Tsiafahy.
Mwanajeshi mmoja wa Madagascar, Kanali Patrick Rakotomamonjy, na washirika wengine wanashukiwa kuhusika, alisema.
Kulingana na Ramanantsoa, waendesha mashtaka wamewashtaki washukiwa kwa kusambaza taarifa potofu ili kuvunja amani, njama ya kuharibu miundombinu ikiwemo nyaya za umeme, pamoja na njama ya uhalifu.
Kundi la WhatsApp
Mamlaka zinasema kundi hilo awali lilikuwa limepanga kutekeleza njama yao Aprili 18, ikiwemo kukata umeme, kutatiza usafiri, kuchochea maafisa wa usalama na kutaka vijana waandamane.
Waendesha mashtaka wameeleza ushahidi wa kundi la WhatsApp linaloitwa ‘‘tolom-piavotan'ny olom-banona" ("Mapinduzi ya Raia Majasiri"), ambayo wanasema lilitumika kupanga njama hiyo.
Wizara ya mambo ya nje inasema Balozi wa Ufaransa nchini humo Arnaud Guillois ametakiwa kufika kwa mamlaka ili aelezwe kuhusu uamuzi juu ya afisa wa ubalozi. Haikumtambua afisa huyo au kueleza alichokifanya.
Reuters haikuweza kuwasiliana na washukiwa moja kwa moja au kufahamu walipo wanasheria wao.
Rakotomamonjy anasubiri kufikishwa mbele ya jaji. Washukiwa wengine wawili wanafuatiliwa, huku waendesha mashtaka wakisema hawaonekani kama walikuwa miongoni mwa waliopanga njama.





















