Nchi jirani zimeimwagia sifa Tanzania kufuatia mchango wa sekta madini wa nchi hiyo katika kukuza pato la taifa (GDP), huku nchi jirani hizo, zikielezea nia ya kujifunza mafanikio ya usimamizi wa sekta hiyo.
Wakizungumza katika Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji wa Madini unaofanyika jijini Nairobi, mawaziri mbalimbali wa madini wa Afrika walitambua hatua kubwa zilizopigwa na Tanzania katika kuifanya sekta ya madini kuwa mhimili wa uchumi.
Waziri wa Madini wa Kenya Hassan Ali Joho, ameitaja Tanzania kama mfano bora wa kuigwa kikanda, akisisitiza umuhimu wa kukuza na kuimarisha sekta ya madini barani Afrika.
Kwa upande wake, Waziri Waziri wa Petroli na Rasilimali Madini wa Somalia Dahir Shire Mohamed, amesema kuwa serikali yake inaichukulia Tanzania kama mfano halisi katika kujenga mifumo imara ya usimamizi wa rasilimali madini.
Akizungumza katika mdahalo maalum wa mawaziri hao, Waziri wa Madini wa Tanzania, Anthony Mavunde, amesema mafanikio hayo yametokana na uongozi thabiti wa kiongozi wa nchi hiyo, Samia Suluhu Hassan, ambaye kwa mujibu wa waziri huyo, ameweka mazingira wezeshi ya uwekezaji, kuimarisha usimamizi wa rasilimali, na kusukuma mbele ajenda ya kuongeza thamani ya madini.
Hapo awali, wakati akifungua mkutano huo, Rais William Ruto wa Kenya, amezitaka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na bara zima la Afrika, kuunganisha nguvu katika kuongeza thamani ya rasilimali madini ili kuongeza tija na ushindani wa ukanda huo katika soko la dunia.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Uwekezaji Tanzania ya Mwaka 2025, thamani ya mtaji wa uwekezaji katika Sekta ya Madini imeongezeka hadi kufikia dola za Marekani bilioni 9.79 kwa mwaka 2024, kutoka dola bilioni 9.15 za mwaka 2023 na dola bilioni 8.64 za mwaka 2022.


















