Wizara ya Ulinzi ya Urusi imedai kuwa vikosi vyake vya Afrika vilihusika kuzuia jaribio la mapinduzi la Aprili 25, nchini Mali.
Kupitia taarifa yake iliyotolewa siku ya Jumanne, wizara hiyo ilisema kuwa vikosi vyake vilihusika kuzuia jaribio hilo.
"Wakati wa mpambano mkali, vikosi vya Afrika vilijibu mashambulizi kwa uhakika na kuwazidi nguvu maadui," ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Kauli hiyo inakuja huku kukiwepo na mfululizo wa mashambulizi yaliyotaribiwa na vikundi vya silaha, vyenye mahusiano na al-Qaeda, kama vile JNIM na kile cha Tuareg.
Katika taarifa iliyosomwa siku ya Jumapili na Jenerali Issa Ousmane Coulibaly, serikali ya mpito ya Mali ilithibitisha kifo cha waziri wake wa ulinzi, Sadio Camara wakati wa mashambulizi hayo.
Kulingana na taarifa hiyo, muuaji wa kujitoa mhanga alielekeza gari lililokuwa limejaa vilipuzi, kuelekea kwenye makazi ya waziri huyo.
Inaripotiwa kuwa, Camara alipambana na watu hao kabla ya kujeruhiwa vibaya na baadaye, kupoteza maisha.


















