| Swahili
AFRIKA
2 dk kusoma
Ghana yawaondoa mamia ya raia wake Afrika Kusini kufuatia vurugu za chuki
Wizara ya mambo ya nje inasema Rais John Dramani Mahama ameidhinisha mpango huo wa kuwaondoa raia wake 300 kutoka Afrika Kusini.
Ghana yawaondoa mamia ya raia wake Afrika Kusini kufuatia vurugu za chuki
Kumekuwa na maandamano dhidi ya wahamiaji nchini Afrika Kusini. / AP

Siku ya Jumanne Ghana ilitangaza kuwa inawaondoa raia wake 300 kutoka nchini Afrika Kusini, baada ya kuongezeka kwa matukio ya chuki dhidi ya raia wa kigeni kote nchini katika wiki za hivi karibuni.

Katika ujumbe kwenye mtandao wa X, Waziri wa Mambo ya Nje Samuel Okudzeto Ablakwa amesema Rais John Dramani Mahama ameidhinisha mpango huo.

"Raia hawa wa Ghana waliopatwa na matatizo walikuwa tayari wameshazingatia maelekezo ya Wizara ya Mambo ya Nje na kujisajili na Ubalozi wetu mjini Pretoria ili warudishwe nyumbani kutokana na mashambulizi ya chuki ya sasa," aliandika.

"Serikali ya Ghana itaendelea kulinda maslahi ya raia wake ndani na nje ya nchi."

Maandamano dhidi ya wahamiaji

Maamuzi haya yanakuja baada ya maandamano dhidi ya wahamiaji nchini Afrika Kusini, pamoja na madai ya mashambulizi na vitisho dhidi ya raia wa mataifa mengine ya Afrika.

Nigeria na Ghana wote wameeleza wasiwasi wao kuhusu hali hiyo.

Hata hivyo, serikali ya Afrika Kusini, imekanusha madai ya chuki.

"Raia wa Afrika Kusini hawana chuki," msemaji wa rais Vincent Magwenya aliwaambia waandishi wa habari wiki iliopita.

"Mlichokiona ni baadhi ya watu tu wakiandamana, ambalo linakubalika kulingana na katiba yetu."

Magwenya alisema Afrika inahitaji kukabiliana na mizozo, ukosefu wa usalama na hali ya "utawala mbaya" ambayo ndiyo imesababisha watu kuhama kote katika bara.

CHANZO:TRT Afrika Swahili