Mahakama ya Afrika Kusini imetupilia mbali maamuzi ya bunge la nchi hiyo ya kubatilisha maamuzi ya kuanzisha mchakato wa kumuondoa madarakani kiongozi wa nchi hiyo, Cyril Ramaphosa kufuatia kashfa ya wizi wa zaidi ya Dola milioni 4.
Ramaphosa anatuhumiwa kukwepa mamlaka za kodi za nchi hiyo, kuhusika na wizi wa fedha za kigeni ambazo baadaye alizificha kwenye ranchi yake iliyopo Kaskazini mwa Jimbo la Limpopo.
Jopo huru la nchi hiyo, lilisema kuwa, huenda kiongozi huyo akawa ametenda makosa ya kihalifu.
Hata hivyo, mwaka 2022, Bunge la nchi hiyo ambalo lilikuwa na idadi kubwa ya wanachama wa chama cha National Congress, liligoma kuanzisha mchakato wa kumuondoa kiongozi huyo madarakani.
Maamuzi ya mahakama hiyo, yanafuatia malalamiko yaliyotolewa na chama cha mrengo wa kushoto cha Economic Freedom Fighters (EFF), kinachoongozwa na Julius Malema.



















