Serikali ya Syria imegundua uwepo wa mabaki yanayohusishwa na mpango wa silaha za kemikali wa aliyekuwa mtawala wa nchi hiyo Bashar al-Assad, ikiwemo silaha za kemikali zinazofanana na zile zilizotumika katika mashambulizi ya kemikali Mashariki mwa Ghouta na Hama, kwa mujibu wa mwakilishi wa Syria katika Shirika la Kuzuia Matumizi ya Silaha za Kemikali (OPCW).
Shirika la habari la serikali nchini Syria SANA limeripoti Jumanne kwamba utafiti na uchunguzi unaoendelea umetambua maeneo yanayohusiana na mpango huo.
Kwa mujibu wa taarifa, wataalamu wa Syria waliobobea katika kemikali za sumu wamepata silaha za kurushwa angani na ardhini sawa na zile zilizotumika katika mashambulizi yaliyofanywa mwaka 2013 na 2017 na utawala ulioondolewa madarakani.
Mamlaka pia imegundua zana zinazotumika kuzalisha gesi ya sarin, pamoja na mitambo ya kuchanganyia kemikali nyengine.
Maeneo yaliyodhibitiwa
Mwakilishi wa Syria katika Shirika la OPCW amesema silaha zote zilizoshikwa, pamoja na vitendea kazi na kemikali zimehamishwa katika eneo maalum linalotumika kuhifadhi kemikali.
Taarifa hiyo imesema serikali imepata mabomu 54 ya angani yanayofanana na yale yaliyotumiwa katika mashambulizi ya mwaka 2017 katika eneo la Latamneh katika jimbo la Hama, pamoja na silaha za ardhini zinazofanana na zile zilizotumika mwaka 2013 Mashariki ya Ghouta.
Serikali ya Syria pia imetangaza kukamatwa kwa watu 18 wanaodaiwa kuhusika na mpango wa silaha za kemikali katika utawala uliopita.
Waliokamatwa, imeripotiwa miongoni mwao ni pamoja na maafisa wa jeshi, waliokuwa wataalamu wa Kituo cha Sayansi na Utafiti na maafisa kutoka kitengo cha ulinzi wanaohusika na mpango wa silaha za kemikali.
Utawala wa Assad umetuhumiwa mara kadhaa na mashirika ya kimataifa na serikali za nchi za magharibi kwa kutumia silaha za kemikali wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria.














