Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) siku ya Jumatano alitoa wito wa kusitishwa mapigano mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ili kutoa fursa kwa mlipuko wa Ebola kudhibitiwa, akisema mapigano yamesababisha watu wengi kuondolewa katika makazi yao na kuongeza maambukizi katika kambi zilizojaa watu.
Aina ya Ebola ya Bundibugyo, ambayo haina chanjo au tiba, ilitangazwa kuwa dharura kimataifa na WHO mapema mwezi huu na maambukizi yamekuwa yakiongezeka.
"Mashariki mwa DRC sasa inakabiliwa na magonjwa na mapigano huku kukiwa na mlipuko wa Ebola katika mkoa wa Ituri ambao si rahisi kudhibitiwa," alisema Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus, ambaye anatarajiwa kusafiri kuelekea eneo hilo wiki hii.
"Hatuwezi kujenga imani ya jamii au kuwatenga wagonjwa huku mabomu yanawashambulia. Tunatoa wito kwa wote wanaopigana kukubaliana kusitisha mapigano ili mlipuko uweze kudhibitiwa," alisema kwenye mtandao wa X.
Maambukizi zaidi 900 yamerekodiwa
Maambukizi zaidi ya 900 na vifo zaidi ya 200 vimeripotiwa kufikia sasa katika mikoa mitatu mashariki mwa DRC ikiwemo mkoa wa Kivu Kaskazini, inayodhibitiwa na waasi wa M23, na mkoa wa Kivu Kusini.
Shirika la misaada la Save the Children lilisema Jumatano kuwa robo ya vifo vilivyothibitishwa viikuwa ni vya watoto, likitoa wito wa juhudi za kinga kuongezwa.
Mapigano yameendelea mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo licha ya juhudi za upatanishi zinazoongozwa na Marekani na wengine, na mamilioni ya watu wameondolewa katika makazi yao. Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia wakimbizi linasema vituo vya muda katika eneo la West Nile la Uganda linalopakana na DRC vimejaa maradufu, nyaraka zimeonesha.
Mashirika ya misaada yanapeleka wahudumu na vifaa mashariki mwa DRC lakini mashambulizi kwa wahudumu wa afya kutokana na jamii kutoamini yamekwamisha juhudi hizo, wanasema. Kufikia sasa, wafadhili wameahidi karibu dola milioni 500 kusaidia katika mlipuko huo lakini bado hazijatolewa, kulingana na maafisa wa afya.

















