Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan Jumatano ameadhimisha sikukuu ya Waislamu ya Eid-al Adha, au Eid ya Kuchinja.
Katika ujumbe wake, Erdogan ameielezea Eid al-Adha kama “baraka za kiroho” na kusema kuwa anatarajia sikukuu hiyo italeta mambo mazuri kwa Uturuki, taifa la Uturuki, ulimwengu wa Kiislamu, na binadamu kwa jumla.
“Kwa ndugu zetu wote ambao wanasherehekea sikukuu hii kwa huzuni, uchungu, katika pande tofauti, hasa wale waliopo Gaza, natanguliza ujumbe wangu wa umoja kwa niaba yangu na taifa langu, na nawapongeza katika siku ya Eid al-Adha,” amesema.
Mamilioni nchini Uturuki leo Jumatano wameswali Eid ikiwa ni siku ya kwanza ya mapumziko.
Pia alipozungumza na waandishi wa habari katika msikiti wa Camlica jijini Istanbul baada ya swala ya Eid, Erdogan amesema sikukuu za dini zinatakiwa kuimarisha umoja na kusaidiana.
“Zaidi ya yote, sikukuu ni siku za kupendana, kuheshimiana, umoja na mshikamano," amesema.
Kiongozi huyo wa Uturuki amesema hali ya Gaza imetia doa katika sherehe hizi za Kiislamu nchini Uturuki na duniani kote.
Erdogan amemkashifu Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, na kumuita "katili" na kuonesha matumaini kwamba ulimwengu wa Kiislamu utaungana kupinga vitendo vya Israel dhidi ya Gaza.
"Pia naamini kwamba, yule katili anayejulikana kama Netanyahu atapata funzo muhimu katika mikono ya ulimwengu wa Kiislamu," amesema.
Uturuki imekuwa ni moja ya nchi zinazopinga vikali unyanyasaji wa kijeshi wa Israel dhidi ya Gaza, huku Rais Erdogan mara kwa mara akitaka kusitishwa kwa mapigano, kufikishwa kwa misaada ya kibinaadamu, na Israel kuwekewa shinikizo la kimataifa.
Kauli yake inakuja wakati ambapo Waislamu duniani wanaadhimisha sikukuu ya Eid al-Adha huku kukiwa na hali ya wasiwasi ya kibinadamu Gaza na eneo lote la Mashariki ya Kati.
Sikukuu hii ni maadhimisho ya Nabii Ibrahim alipokuwa tayari kumtoa kafara mtoto wake kutokana na amri ya Mwenyezi Mungu, kabla ya kupewa kondoo kumtoa kafara.
Waislamu wanachinja wanyama na kutoa sadaka ya nyama kwa ndugu, jamaa na marafiki.


















