Miili ya wahamiaji wasiopungua 15, akiwemo msichana mdogo, imesombwa na maji kando ya pwani ya mashariki ya Mediterania ya Libya baada ya mashua inayoaminika kuwa na watu wapatao 61 kupinduka, vyanzo vya usalama, jeshi la wanamaji na matibabu vilisema Jumamosi, katika mkasa wa hivi punde kwenye mojawapo ya njia mbaya zaidi za wahamiaji duniani.
Miili hiyo iliopolewa kutoka maeneo kadhaa kando ya pwani karibu na Tobruk, karibu na mpaka wa Libya na Misri.
Maafisa wawili wa usalama walisema mabaki hayo yalikuwa yameoza vibaya, ikiashiria kuwa yalikuwa majini kwa siku kadhaa, na kuonya kuwa miili zaidi bado inaweza kupatikana.
Kulingana na chanzo cha jeshi la wanamaji la Libya, manusura 10 waliambia mamlaka meli hiyo ilikuwa imebeba takriban wahamiaji 61 ilipozama.
Picha zilizotolewa na Shirika la Red Crescent la Tobruk zilionyesha watu waliojitolea wakiwa wamevalia suti za kujikinga wakichukua miili kutoka kwenye ufuo wa mawe kabla ya kuwaweka kwenye mifuko nyeupe kwa ajili ya mazishi.
Libya imekuwa moja ya nji kuu kwa wahamiaji wanaojaribu kuvuka kwa hatari kuelekea Ulaya tangu maasi ya 2011 ambayo yalimwondoa Muammar Gaddafi.
Nchi hiyo pia inavutia maelfu ya wahamiaji wanaotafuta kazi katika uchumi wake unaotegemea mafuta, lakini hali ya kutokuwa na utulivu inayoendelea imechochea mitandao ya ulanguzi wa binadamu ambayo inawalenga watu walio katika mazingira magumu.
Maafa ya hivi punde yanaongeza idadi ya vifo vya wahamiaji katika eneo la kati la Mediterania.
Mapema wiki hii, mamlaka ya Libya ilizika wahamiaji wengine 15 ambao miili yao ilisombwa ufukweni mashariki mwa Tripoli, huku makundi tofauti ya uokoaji yakiripoti kuwa takriban watu 51 wanahofiwa kufariki au kutoweka baada ya boti nyingine kupinduka mashariki mwa Libya tarehe 12 Juni.
Shirika la Kimataifa la Uhamiaji limeelezea mara kwa mara eneo la kati la Mediterania kama mojawapo ya njia mbaya zaidi za wahamiaji duniani, huku mamia ya wahamiaji wakiripotiwa kufariki au kutoweka tayari mwaka huu.










