Zaidi ya 85% ya ugavi wa damu duniani sasa unatoka kwa wafadhili wa hiari, wasiolipwa, na hivyo kuashiria hatua kubwa katika jitihada za kimataifa za kufanya uchangiaji damu kuwa salama zaidi.
Lakini Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) linaonya kwamba mamilioni ya watu, haswa katika nchi zenye mapato ya chini, bado wanatatizika kupata damu na bidhaa zinazookoa maisha wakati wanazihitaji.
Takwimu mpya za WHO, zilizotolewa kabla ya Siku ya Wachangia Damu Duniani mnamo Juni 14, zinaonyesha kuwa uchangiaji damu duniani uliongezeka kwa karibu 19% kati ya 2013 na 2023, na kufikia wastani wa uchangiaji wa damu milioni 120.4.
Hata hivyo, faida zinabaki kutofautiana.
Serikali ziimarishe mifumo ya kukusanya damu
Ingawa nchi zenye kipato cha juu zinachangia asilimia 15 tu ya watu duniani, zinakusanya asilimia 36 ya damu zote, huku mataifa mengi ya kipato cha chini yakiendelea kukabiliwa na uhaba wa muda mrefu ambao unahatarisha wanawake wenye kuvuja damu sana wakati wa kujifungua, watoto wenye upungufu wa damu, waathiriwa wa ajali, wagonjwa wa saratani na watu wanaoishi na matatizo ya damu kama vile ugonjwa wa sickle-cell na thalassemia.
"Hakuna anayepaswa kufa kwa sababu damu salama haipatikani inapohitajika," alisema Dk Deusdedit Mubangizi, Mkurugenzi wa Sera na Viwango vya Dawa na Bidhaa za Afya wa WHO. “Takwimu hizi zinaonyesha maendeleo ya kutia moyo, hasa katika kuongezeka kwa idadi ya wachangiaji damu bila malipo kwa hiari ulimwenguni, msingi wa usambazaji wa damu salama na endelevu, lakini pia zinatukumbusha kwamba mahali anapoishi mtu bado anaweza kuamua ikiwa anaweza kupata damu anayohitaji,’’ aliongeza.
Shirika hilo linazitaka serikali kuimarisha mifumo ya kitaifa ya damu, kuboresha uchunguzi na upimaji, kupanua programu za wachangiaji wa hiari na kuwekeza katika huduma dhabiti za utiaji damu ili kuhakikisha upatikanaji wa damu salama kwa wote kama sehemu ya juhudi pana za kufikia huduma ya afya kwa wote.
Damu salama inategemea utawala thabiti na udhibiti wa mifumo ya uchangiaji damu, sambamba na ushiriki endelevu na kujitolea kwa wachangiaji wa damu.
Uchambuzi wa WHO unaonyesha kuwa karibu theluthi moja ya nchi bado hazina sheria maalum ya kuhakikisha usalama na ubora wa damu na bidhaa za damu.
Zaidi ya uniti milioni 120 za damu hutolewa ulimwenguni kila mwaka, lakini Shirika la Afya Ulimwenguni linasema hii bado haitoshi kukidhi mahitaji ya kimataifa, na hivyo kuacha mamilioni ya wagonjwa bila upatikanaji kwa wakati wa kutiwa damu kuokoa maisha.















