Umoja wa Mataifa sharti ufanyiwe mabadiliko ili kuongeza uwakilishi wa Afrika, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres siku ya Jumatatu katika upanuzi wa ofisi ya UN nchini Kenya.
Guterres mara kadhaa amekuwa akiitisha mabadiliko ili kuipa Afrika na maeneo mengine uwakilisha mzuri katika Umoja wa Mataifa.
Hata hivyo, ombi hilo halijafanikiwa sana kwa sababu linataka wajumbe watano wa kudumu katika Baraza la Usalama, ambao ni Uingereza, China, Ufaransa, Urusi na Marekani, kukubali kupunguza nguvu zao.
"Tunahitaji mabadiliko ya kina...taasisi za dunia zinazoakisi ulimwengu kama ulivyo leo, sio kama ulivyokuwa miaka 80 iliyopita, na hii inajumuisha Baraza la Usalama, ambapo hali ya kihistoria ya kutokuwa na usawa iliinyima Afrika kiti cha kudumu," Guterres amewaambia waandishi wa habari.
Mabadiliko ni lazima
Alipoulizwa na AFP kama kuna ramani halisi kuelekea mabadiliko katika Baraza la Usalama, Guterres alisema itakuwa "ngumu."
"Lakini kuna hatua ambazo tayari zinaelekea njia sahihi," amesema.
"Ni muhimu kusema kwamba mabadiliko ni lazima, kwa sababu ya mabadiliko ya kisiasa tunayoshuhudia, ni taabu sana katika dunia ya sasa kupata amani na utulivu, ni taabu sana, hivyo tunataka Baraza la Usalama lenye uwezo wa kufanya kazi," amesema Guterres.
Guterres alikuwa nchini Kenya kushuhudia uanzishwaji wa upanuzi wa ujenzi wa ofisi za Umoja wa Mataifa jijini Nairobi wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 340- moja wapo ya jitihada za kupunguza gharama kwa kuhamisha wafanyakazi kutoka ofisi za New York na Geneva.
'Hatua ya kupunguza gharama'
"Ni sehemu rahisi kuliko nyengine...Ni hatua nzuri kwa Umoja wa Mataifa," amesema Guterres.
Ofisi hiyo imeanza kama kituo cha kikanda cha ofisi ya UN ya mazingira lakini imepanuka na kuwa na zaidi ya ofisi 80 na zaidi ya wafanyakazi 4,000.
Marekani imekata ufadhili wake kwa UN chini ya Rais Donald Trump, na kutishia kupunguza zaidi, hivyo kulifanya shirika hilo kupunguza gharama.
















