Rais wa zamani wa Botswana Festus Mogae, aliyeongoza taifa hilo la kusini mwa Afrika kwa mwongo mmoja kuanzia 1998, na anakumbukwa kwa kukabiliana na maambukizi ya UKIMWI ,amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 86, ofisi ya rais ilisema siku ya Ijumaa.
Mwanauchumi aliyepata mafunzo yake nchini Uingereza, alichangia ukuaji wa uchumi wa nchi hiyo katika mihula yake miwili aliyokuwa uongozini.
"Kama taifa, tuna huzuni kwa kumpoteza kiongozi muhimu na aliyetumikia watu ambaye dhamira yake kwa watu wa Botswana ilikuwa thabiti kipindi chote cha uhai wake," Rais wa sasa Duma Boko alisema.
Serikali imetangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa, ambapo bendera zitapepea nusu mlingoti.
Mogae aliingia madarakani kama rais wa awamu ya tatu baada ya Ketumile Masire kung’atuka, ambapo awali alikuwa makamu wake wa rais.
Mshindi wa tuzo ya Ibrahim
Alirithiwa na Ian Khama 2008, mkuu wa majeshi wa zamani na mtoto wa rais wa kwanza wa Botswana.
Mogae anakumbukwa kwa kukabiliana na maambukizi ya UKIMWI wazi katika kipindi ambacho Botswana ilikuwa na maambukizi mengi zaidi duniani.
2008, alishinda tuzo ya Ibrahim kwa uongozi wake uliosaidia nchi kuwa salama na kupata mafanikio wakati wakipitia changamoto.
Baada ya kustaafu, alikuwa mwenyekiti wa tume ya pamoja ya Kufuatilia na Kutathmini, akiwa na jukumu muhimu la kusimamia mchakato wa amani wa Sudan Kusini.


















