Takribani watu 100 wameuawa katika moto uliotokea kwenye sherehe ya harusi Iraq

Takribani watu 100 wameuawa katika moto uliotokea kwenye sherehe ya harusi Iraq

Pia watu 500 walijeruhiwa katika tukio hilo wilaya ya Al-Hamdaniya katika mkoa wa Nineveh
Angalau watu 100 wameuawa katika moto uliotokea kwenye sherehe ya harusi kaskazini mwa Iraq | Picha: AA

Watu wasiopungua 100 walifariki katika moto uliotokea wakati wa sherehe ya harusi katika mkoa kaskazini wa Nineveh nchini Iraq, mamlaka za eneo hilo zilisema Jumatano.

Watu wengine 500, ikiwa pamoja na bibi na bwana harusi, walijeruhiwa kwenye moto huo, uliozuka katika Ukumbi wa Harusi wa Al Haytham katika wilaya ya Al-Hamdaniya, vyombo vya habari vya eneo hilo viliripoti, vikimnukuu Ahmed Hamdani, Naibu Mkurugenzi wa Idara ya Afya ya Mosul.

Kulikuwa na watu 800 kwenye ukumbi wa harusi wakati moto ulipozuka, kulingana na ripoti.

Shirika la Habari la Iraq (INA) limesema kuwa moto huo ulisababishwa na fataki, mishumaa, na vifaa vingine vilivyotumika wakati wa tukio hilo.

Magari ya zimamoto na magari ya wagonjwa kutoka mikoa inayozunguka yalipelekwa kwenye eneo hilo.

Waziri wa Mambo ya Ndani Abdul Amir Al-Shammari pia alielekea kwenye eneo hilo.

Picha za video za moto huo zilisambazwa sana kwenye mitandao ya kijamii, zikionyesha wakati moto ulipotokea wakati bibi na bwana harusi walipokuwa wakicheza, pia zikionyesha watu wakikimbia huku na kule kwa hofu.

AA