Jimmy Carter, rais wa 39 wa Marekani, amefariki dunia, gazeti la Atlanta Journal-Constitution liliripoti. Alikuwa na umri wa miaka 100.
Mwanachama wa Democrat, alikuwa rais kuanzia Januari 1977 hadi Januari 1981 baada ya kumshinda rais aliyekuwa madarakani wa chama cha Republican Gerald Ford katika uchaguzi wa Marekani wa 1976.
Carter aliondolewa madarakani miaka minne baadaye wakati wapiga kura walipompigia kura nyingi mpinzani wake wa chama cha Republican Ronald Reagan, mwigizaji wa zamani na aliyekuwa gavana wa jimbo la California.
Carter aliishi miaka mingi baada ya kustaafu kuliko rais mwingine yoyote wa Marekani. Muhula wake mmoja ulikuwa na mafanikio makubwa kama upatanishi wa 1978 wa Camp David kati ya Israel na Misri.
Lakini ulikumbwa na mdororo wa kiuchumi, na watu kutokuwa na imani naye na matatizo ya kutekwa nyara kwa raia wa Marekani nchini Iran, tatizo lililokwamisha siku zake 444 za mwisho madarakani.
Katika miaka ya hivi karibuni, Carter alisumbuliwa na maradhi kadhaa ikiwemo saratani ya ngozi ambayo ilisambaa hadi kwenye ini na ubongo. Carter aliamua kupata huduma itakayomuezesha kuishi siku zake za mwisho vizuri Februari 2023 badala ya kupata matibabu zaidi.
Mke wake, Rosalynn Carter, alifariki dunia Novemba 19, 2023, akiwa na umri wa 96. Alionekana anaumwa wakati akiadhimisha kumbukumbu ya kifo cha mkewe akiwa kwenye kiti magurudumu.
Kwa miongo kadhaa, Carter alijihusisha na miradi ya kusaidia watu. Alipewa tuzo ya Nobel ya amani 2002 kwa kutambua mchango "wake wa kuendelea kutafuta amani na kutatua mizozo ya kimataifa, kuhamasisha demokrasia na haki za binadamu, na kuimarisha masuala ya uchumi na kijamii."