Raia wa Palestina akifuatilia habari katika simu yake kuhusu makubaliano kati ya Israeli na Hamas ya kusitisha mapigano, akiwa katika eneo la Dura, West Bank, Januari 15, 2025. / Picha: Reuters

Baada ya miezi 15 ya mashambulizi ya Israeli Gaza, makubaliano muhimu yamefanyika: Kundi la ukakamavu la Hamas na Israel wanaripotiwa kukubaliana kuhusu usitishwaji wa mapigano, uliopangwa kuanza Jumapili.

Makubaliano haya muhimu yanajumuisha kusitisha ukatili, kuachiwa kwa mateka, na kubadilishana kwa wafungwa.

Wapatanishi kutoka Qatar, Marekani, Misri na pande nyengine wamekuwa na mchango mkubwa katika kufanikisha makubaliano hayo.

Taarifa zaidi za makubaliano ambazo zinaripotiwa kupitishwa na pande zote mbili bado hazijawekwa wazi.

Hizi ndio taarifa ambazo mpaka sasa zinafahamika kutokana na taarifa iliyotolewa na Rais wa Marekani Joe Biden, kwa mujibu wa wapatanishi wa Qatar na vyombo vya habari.

Awamu ya kwanza: Makubaliano ya wiki sita ambapo Israeli pole pole itaanza kuondoa wanajeshi wake Gaza

Kuachiliwa kwa mateka: Hamas inatarajiwa kuwaachia mateka, zaidi wakiwa wanawake, watoto na wazee, katika kubalidilisha na mamia ya wafungwa wa Kipalestina wanaoshikiliwa na Israeli.

Msaaada wa kibinadamu: Kuongezeka kwa msaada wa kibinadamu Gaza, kuruhusu mamia ya magari ya mizigo katika eneo lililozingirwa.

Kilichopelekea makubaliano?

Waziri Mkuu wa Qatar Sheikh Mohammed bin Abdulrahman al Thani ametangaza makubaliano hayo mjini Doha siku ya Jumatano, akigusia lengo lake ni kumaliza mapigano ya Israeli na kuwasilisha msaada unaohitajika haraka kwa Wapalestina.

Rais wa Marekani Joe Biden alikaribisha mafanikio hayo, akisisitiza umuhimu wa kuunganisha familia na kupeana misaada ya kibinadamu.

Wakati makubaliano hayo yakitoa mwanga wa matumaini, mrengo wa kulia ndani ya muungano wa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu umekosoa makubaliano hayo.

Hamas, katika taarifa yake, wamepongeza mpango huo kama ushindi kwa Wapalestina.

Hata hivyo, uhasama unaendelea huku makubaliano rasmi yakisubiri kuidhinishwa na baraza la mawaziri la usalama la Israel na serikali, huku kura zikitarajiwa Alhamisi.

Hadi wakati huo, mashambulizi mabaya ya anga ya Israel yanaendelea huko Gaza, na kuchukua maisha ya wengi zaidi.

TRT World